Michezo

Shujaa waelekea Amerika kwa duru ya tano ya Raga za Dunia

February 26th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Samuel Oliech wa timu ya Shujaa (aliye juu zaidi) awania mpira na Tavite Veredamu wa Ufaransa katika mechi ya awali. Picha/ Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya wanaume ya Kenya almaarufu Shujaa ilifunga safari ya kuelekea nchini Marekani saa sita kasorobo Jumamosi usiku.

Ndege iliyobeba vijana hao wa kocha Innocent Simiyu ilipitia jijini Doha nchini Qatar kabla ya kuelekea mjini Las Vegas ambapo duru ya tano ya Raga za Dunia itafanyika Machi 2-4, 2018.

Kenya, ambayo inashikilia nafasi ya nane kwa alama 35 ilizopata katika duru nne za kwanza, italimana na Fiji, Ufaransa na Urusi katika mechi za Kundi A.

Mabingwa wa Singapore Sevens mwaka 2016 Kenya wanalenga kumaliza duru zote 10 kwa jumla ya alama 100.

Ina maana kwamba watahitajika kujikakamua vilivyo kutimiza lengo hilo hasa kwa sababu kufikia sasa wako pointi tano nje ya lengo hilo.

Shujaa imeratibiwa kurejea nchini Machi 13 baada ya kushiriki duru ya sita mjini Vancouver nchini Canada hapo Machi 10-11.

Kikosi cha Shujaa – Oscar Ouma (nahodha), Collins Injera, Billy Odhiambo, Andrew Amonde, Daniel Sikuta, William Ambaka, Arthur Owira, Eden Agero, Samuel Oliech (nahodha msaidizi), Jeffery Oluoch, Nelson Oyoo, Eric Ombasa na Sam Muregi.

Ratiba ya Shujaa:

Machi 2

Kenya vs. Ufaransa (3.44pm)

Kenya vs. Urusi (6.45pm)

 

Machi 3

Kenya vs. Fiji (12.36pm)