Shujaa yaaga Singapore Sevens kwa alama 10
Na GEOFFERY ANENE
KENYA imemaliza Raga ya Dunia ya duru ya Singapore Sevens katika nafasi ya saba kwa alama 10 Jumapili.
Shujaa ya kocha Innocent Simiyu sasa inashikilia nafasi ya sita baada ya duru nane za kwanza kwa jumla ya alama 93.
Fiji (alama 145), Afrika Kusini (141), New Zealand (120), Australia (118) na Marekani (93) ziko katika nafasi tano za kwanza, mtawalia.
Zinafuatiwa na Kenya (93), Argentina (92), Uingereza (88), Samoa (55), Scotland (51), Canada (51), Ufaransa (47), Uhispania (45) na Wales (35) nayo Urusi iko mkiani kwenye ligi hii ya mataifa 15 kwa alama 20. Fiji imeng’oa Afrika Kusini juu ya jedwali baada ya kuzima Australia 28-22 katika fainali kali.
Shujaa, ambayo ilipigwa 17-7 katika nusu-fainali ya kutafuta nambari tano hadi nane, iliimarika kutoka nafasi ya saba hadi sita baada ya kunufaika na Argentina kumaliza katika nafasi ya 14 kwa alama mbili.
Wakenya walilemewa na mabingwa wa Cape Town Sevens New Zealand 17-7 kupitia alama za Kurt Baker, Dylan Collier na Trael Joass. Daniel Sikuta alifungia Kenya mguso wa kufutia machozi ulioandamana na mkwaju kutoka kwa Eden Agero.
Shujaa ilifungua siku ya mwisho ya Singapore Sevens kwa kuzidiwa maarifa na mabingwa wa Dubai Sevens Afrika Kusini 24-12 katika robo-fainali.
Ilipata alama za kujiliwaza kupitia kwa Collins Injera aliyefikisha miguso 260 tangu aanze kuchezea Kenya mwaka 2006 baada ya kufunga miguso miwili katika kipindi cha pili. Samuel Oliech alichangia mkwaju mmoja.
Katika siku ya kwanza, Kenya ilipoteza 19-28 dhidi ya Uingereza katika mechi yake ya kwanza ya Kundi B kabla ya kuingia robo-fainali kwa kupepeta Ufaransa 34-0 na Marekani 33-14.