SHWARI: Faraja yarejea baada ya Kenya kupiga Tanzania
Na JOHN ASHIHUNDU
ALIYEKUWA nahodha wa Harambee Stars, Musa Otieno amesema ana matumaini makubwa ya timu hiyo kupata matokeo mazuri dhidi ya Senegal kwenye mechi ya mwisho ya Kundi C Jumapili na kutinga raundi ya 16-bora.
Mbali na ushindi, Harambee Stars yaweza kufuzu kwa hatua hiyo iwapo itapata sare na Senegal kwani itakuwa imefikisha alama nne na kufuzu kama moja ya timu nne zitakazofuzu licha ya kumaliza kama nambari tatu.
Stars pia inaweza kufuzu hata ikishindwa na Senegal, lakini hilo litategemea matokeo ya timu nyinginezo katika makundi yote sita mbali na kuomba kuwa Tanzania isishinde Algeria.
Otieno ambaye ni mmoja wa wachanganuzi wa mechi za AFCON kupitia kwa runinga ya SuperSport moja kwa moja kutoka Afrika Kusini, alisema anafahamu ugumu wa mechi hiyo, lakini anaamini iwapo Stars watacheza kwa bidii jinsi walivyocheza na Tanzania na kupata ushindi wa mabao 3-2, Alhamisi, watafanikiwa.
“Michuano hii si rahisi, kila timu inayojivunia pointi tatu kutokana na mechi mbili kufikia sasa, ina nafasi ya kusonga mbele, Kenya ikiwemo na kila kitu kinawezekana,” alisema Otieno ambaye pia aliwahi kuchezea klabu za nyumbani AFC Leopards, Gor Mahia na Kenya Breweries (sasa Tusker FC), kabla ya kuyoyomea nchini Afrika Kusini kusakata soka ya kulipwa.
“Baada ya kuibwaga Tanzania 3-2, mashabiki wengi wa Harambee Stars wanasubiri kwa hamu, huku wengi wakiipa Stars nafasi sawa mbele ya Senegal, ambayo ilishindwa 1-0 na Algeria, Alhamisi usiku,” aliongeza mlinzi huyo mstaafu.
Hata hivyo, jagina huyo mwenye umri wa miaka 45 alilalamika kuhusu mabeki wa pembeni wa Harambee Stars ambao alidai walikuwa na ulegevu mkubwa. Otieno alimlaumu kocha Sebastien Migne kwa kuamua kumchezesha David Owino “Calabar” kama beki wa kushoto ilhali amezoea kucheza kama beki wa katikati.
Ampongeza kwa kurekebisha makosa
Lakini alimpongeza kwa kurekebisha makosa ya mara kwa mara ambayo walifanya katika mechi ya utangulizi ambayo yalisababisha penalti iliyofungwa na Baghadad Bounedjah, kisha wakalemewa kuzuia kombora la Riyad Mahrez ambalo lilimgonga beki Aboud Omar kabla ya kutinga nyavu.
Otieno alisema katika mechi hiyo, Harambee Stars walikosa kushambulia jinsi walivyoshambulia dhidi ya Tanzania na kupata mabao ya ushindi kupitia kwa Michael Olunga na Johanna Omollo.
Alisema Dennis Odhiambo na Francis Kahata hawakumsaidia Victor Wanyama ipasavyo katika safu ya kati katika mechi ya kwanza, lakini akampongeza kocha kwa kugundua kasoro hiyo na kurekebisha kikosi chake mapema kwa kuwapa watu wengine nafasi hizo.
Kuhusu pambano la ufunguzi dhidi ya Algeria, Otieno alisema wapinzani walitegemea makosa ya mabeki wa Kenya kufunga mabao yao.
“Ni miaka mingi tangu tucheze michuano hii na kila mtu nyumbani ana hamu kuona Stars wakipata matokeo mazuri dhidi ya Senegal na kusonga mbele,” alisema.
Hii ni mara ya sita kwa Harambee Stars kushiriki kwenye michuano hii, baada ya kuwa huko kwa mara ya mwisho 2004.