• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 6:55 PM
SIONDOKI SPURS: Wanyama akariri haiachi klabu yake licha ya uvumi

SIONDOKI SPURS: Wanyama akariri haiachi klabu yake licha ya uvumi

Na JOHN ASHIHUNDU

NAHODHA wa Harambee Stars, Victor Wanyama amesisitiza kwamba haendi popote kinyume na uvumi unaoenea kwamba anajiandaa kuyoyomea nchini Uturuki kuchezea Fenerbahce ama Galatasaray.

Kadhalika kiungo huyo wa klabu ya Tottenham Hotspur amehuzunishwa na mpango wa kujiunga na West Ham, pia ya ligi kuu ya Uingereza (EPL).

Tayari kuna madai kupitia kwa vyombo vya habari kwamba mazungumzo kuhusu kitita cha Sh3 bilioni yamefanyika, ingawa amesisitiza kwamba haendi popote.

“Sitaki kuzungmza kuhusu uvumi unaoendelea. Sijazungumza na timu yoyote na lengo langu ni kubakia hapa kusaidia klabu yangu msimu ujao. Siendi popote kwa sasa,” alisema nyota huyo mwenye umri wa miaka 28.

“Ningali na mkataba na Spurs na ningependa kuuheshimu hadi utamatike.”

Lakini licha ya msimamo wake, uvumi unendelea kurudiwa kwenye vyombo vya habari nchini Uingereza ambako gazeti moja la kila siku limeripoti kwamba staa huyo ambaye alikuwa akitafuta uraia wa taifa hilo hakuweza kuondoka msimu uliopita kwa sababu hajaishi nchini humo kwa zaidi ya miaka sita.

Kwenye ngazi ya klabu yake, Wanyama anakabiliwa na hali ngumu kufuatia kuwasili kwa kiungo mahiri Tanguy Ndombele, Harry Winks na Moussa Sissoko.

Amerejea mazoezini akiwa amechelewa baada ya kushiriki katika michuano ya AFCON akiwa na kikosi cha Harambee Stars na sasa ameanza kuwania nafasi kikosi kwa ajili ya mechi za kirafiki, ikiwemo ya Jumapili dhidi ya Inter Milan.

Habari zaidi kutoka nchini Uturuki zimesema huenda dili ya kuhamia nchini humo ikamalizika siku chache zijazo, ingawa muhula wa uhamisho baina ya klabu za EPL unamalizika Agosti 8, lakini ligi nyingine barani Ulaya, ikiwemo ligi kuu ya Uturuki ni hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Agosti.

Iwapo atajiunga na Galatasaray, Wanyama atakuwa akipokea Sh9,700 milioni kwa wiki, ingawa kuna uwezekano wa kuendelea kubakia klabuni mwake.

Mchezaji wa akiba

Lakini uhakika ni kwamba akibakia Spurs, atakuwa mchezaji wa akiba kwa vile miamba waliowasili ni wakali kwenye safu ya kiungo kumliko.

Wanyama aliichezea Spurs mechi 13 msimu uliopita, huku akianza mara nne katika kikosi cha kwanza.

Wanyama alikuwa katika kikosi cha Spurs kilichocheza fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa barani Ulaya dhidi ya Liverpool mnamo Juni Mosi, jijini Madrid.

Kiungo huyo pamoja na Harry Kane walikuwa wamerejea siku chache tu baada ya kusumbuliwa na majeraha.

Spurs walikuwa na azma na matumaini mengi ya kunyakua taji hilo kwa mara ya kwanza lakini wakachapwa 2-0.

Wakati huo, Pochettino alikumbwa na hali ngumu kupanga kikosi chake ambacho kilikuwa na wachezaji wengi majeruhi.

You can share this post!

Miheso mwingi wa imani Stars itapiga TZ

Kocha alalama kutohusishwa na usajili Spurs

adminleo