SOKA U-14: Kipa wa Quba Rescue Team anayelenga kuwa sumaku langoni
Na PATRICK KILAVUKA
AKIWA langoni bila shaka yeye ni sumaku au komeo kwani hudaka na kuganda na boli mithili ya nyani.
Safari yake ya uchezaji kama mnyakaji ilingoa nanga akicheza timu ya mtaani ya Gully Side FC kabla kupata zizi lipya katika kikosi cha Quba Rescue Team akijumlishwa katika kikosi cha wasiozidi miaka kumi na minne.
Kipa Samuel Karanja, 18, mwanafunzi wa kidato cha nne shule ya upili ya Treasurer, Gitaru, ameichezea shule yake na timu hii ya mtaani kwa matao tofuati.
Mwaka huu, ameikamatia shule yake hadi kiwango cha Kaunti ya Kiambu ambapo alitetea lango kwa kujihami zaidi japo walizabwa na Shule ya Upili Alliance baada ya kukubali goli moja tu dakika za kawaida na mambo kuwa sarevya 1-1 kisha ulazima wa kupata mshindi ukawa uamuliwe kupitia matuta ambapo walitingwa 5-4 japo mechi ilikuwa kali. Hata hivyo, hakufa moyo kwani anajua fika katika kandanda kuna kukubali matokeo.
Mlinda lango huyu akishika wala kupangua mpira, huwezi kuamini kwa sababu hupiga mbizi kama nyani mzoefu.
Anavalia jezi nambari moja na ni tegemeo la timu yake ambayo inafanyia mazoezi chuo cha Kiufundi cha Kirangari, Nyathuna.
Kwa kushirikiana na wachezaji wenza uwanjani, hukakikisha ngome iko imara kama kigongo na huwa hubabaiki mithili ya kumbekumbe kwenye mtego wa ndege wakati wapinzani wananuia kuvizia lango kwa mashuti kwani, hukaa chonjo langoni aidha kuudaka au kuupangua.
Chini ya kocha wa Sammy Ngotho, mnyakaji mpira huyu anasema amepigwa msasa na kuimarisha mbinu ya kuwajibikia lango.
“Huwa ananihimiza kuwa mjasiri langoni tushinde tusishinde kwani hayo yote in kawaida katika soka,” asema Karanja ambaye amedakia timu hii katika michuano ya ligi ya FKF, Kaunti Ndogo ya Kabete.
Anakiri kwamba mchuano ambao ulikuwa wa mawimbi kwake, ulikuwa dhidi ya Kanjeru Youth
ambapo ngome yao ilivuja na kumpelekea kuviziwa mara matatu.
Karanja anasema kipawa chake kimefuata mkondo wa mzazi Kennedy Kimani na kuongezea kwamba, mchezo wa kabumbu umempatia fursa ya kupepea katika ulimwengu wa soka na kipawa chake kunawiri huku akiwa na matumaini ya kufanya vyema.
Katika fani ya soka, anahusudu mshikaji boli Jordan Pickford ambaye anaichezea timu ya Everton ughaibuni kutokana na upigaji mbizi wake akinyaka boli na bidii yake ya mchwa katika kulinda lango pasipo kukata tamaa na kupigana kufa kupona kuhakikisha timu inafanya kweli mchezoni.
Ingawa yeye ni kipa, anasema anapenda pia jinsi kiungo Francis Kahata anavyosakata boli akijituma uwanjani.
Kwa vile yeye ni mtahiniwa, anajaribu kuwianisha masomo na boli kwa kutia bidii masomoni kwa kuhakikisha anafanya kila kazi ya ziada kabla kujitosa uwanjani kujinoa hadi saa kumi na mbili.
Mafanikio ambayo ameyapata kutokana na kupambana katika mchezo huo, ni kupokea gluvu na tunu baada ya kufanya vyema katika mashindano ya Kaunti ambapo timu yake ilibuka bingwa wa kaunti ndogo ya Kabete kwa kuibwaga Congo Boys 3-0 akiwa mchumani.
Angependa kusomea uhandisi wa stima na anawarai vijana kujihusisha na michezo kustawisha talanta zao na kuzikuza.