Son Heung-min arejea Spurs baada ya kutumikia jeshi la Korea Kusini kwa wiki tatu
Na CHRIS ADUNGO
FOWADI Son Heung-min wa Tottenham Hotspur amerejea jijini London, Uingereza baada ya kukamilisha kipindi cha lazima cha huduma kwa taifa la Korea Kusini.
Son alihudumia Jeshi la Korea Kusini kwa kipindi cha majuma matatu na akawa miongoni mwa watumishi watano bora zaidi katika muda huo.
Nyota huyo mwenye umri wa miaka 27 hahitajiki kujitenga kwa siku 14 jijini London isipokuwa akipatikana na virusi vya corona.
Atakuwa huru kuungana na wachezaji wenzake wa Tottenham wakati wa kipindi cha mazoezi cha Jumatatu ya Mei 18, 2020.
Kwa sasa, wachezaji wa klabu mbalimbali za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) wanajifanyia mazoezi kivyao kwa muda usiozidi dakika 75 chini ya mwongozo wa kanuni mpya za afya.
Ni matarajio ya mashabiki na wadau wengine wa soka ya Uingereza kwamba kivumbi hicho kitaanza kutandazwa upya msimu huu mnamo Juni 12, 2020.
Vijibendera kwenye kona za uwanja, mipira, milingoti na miamba ya malango na maeneo yote ya kuchezea yatakuwa yakinyunyiziwa dawa baada ya kila kipindi cha mazoezi.
Son amepona kabisa kutokana na jeraha la mkono uliovunjika mwishoni mwa msimu jana. Isingalikuwa kwa janga la corona ambalo lilisababisha shughuli zote za soka kusimamishwa nchini Uingereza kuanzia Machi 2020 Son angalisalia nje kwa kipindi chote kilichosalia katika kampeni za muhula huu.
Son amewezeshwa kutoa huduma zake kwa taifa la Korea Kusini bila ya zoezi hilo kuathiri taaluma yake ya usogora.
Alipunguziwa kipindi cha kawaida cha kulitumikia taifa kwa kipindi cha miezi 21 baada ya kuwa sehemu ya timu ya taifa ya Korea Kusini iliyonyakua ubingwa wa Michezo ya bara Asia mnamo 2018.
Kutokana na ufanisi huo wa timu ya taifa ya Korea Kusini, Son alihitajika sasa kuitumikia nchi yake kwa kipindi cha wiki tatu pekee.