Spurs, Foxes wapata meno ya kung’ata tena
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
KLABU za Tottenham Hotspur na Leicester City zilimaliza ukame wa kutoshinda kwenye Ligi Kuu baada ya kung’ata Norwich 2-1 na West Ham 4-1 mtawalia, Jumatano.
Nambari tatu Leicester ilikuwa imepepetwa 2-1 dhidi ya Burnley na Southampton kabla ya kunyamazisha West Ham kupitia mabao ya Ayoze Perez (mawili bao moja likiwa penalti), Harvey Barnes na Ricardo Pereira. Mark Noble alifungia West Ham bao la kujifariji kupitia penalti.
Tottenham ya kocha Jose Mourinho, ambayo inashikilia nafasi ya sita, haikuwa imepata ushindi katika mechi nne zilizopita baada ya kutoka sare dhidi ya Watford 0-0 na Norwich 2-2 na kupoteza dhidi ya Southampton na viongozi Liverpool kwa bao 1-0.
Ililemea Norwich kupitia mabao ya Dele Alli na Heung-Min Son. Norwich ilijiliwaza na bao kutoka kwa Teemu Pukki.
Aidha, kocha Brendan Rodgers anatumai mshambuliaji Jamie Vardy hatakuwa mkekani kwa muda mrefu baada ya mfungaji huyo bora wa Leicester kutoka uwanjani akichechemea dhidi ya West Ham.
Vardy aliumia akikimbilia pasi katika kipindi cha kwanza uwanjani King Power.
Alipokea matibabu kwa dakika kadha kabla ya kujaribu kuendelea na mechi, lakini baada ya sekunde chache alijishika mguu na kukaa chini.
Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33 hakuweza kuendelea na mechi na nafasi yake ikatwaliwa na Kelechi Iheanacho.
Vardy anaongoza ufungaji wa mabao kwenye Ligi Kuu msimu huu baada ya kutikisa nyavu mara 17 na itakuwa pigo kubwa akikosekana kwa muda mrefu.
Hata hivyo, akizungumza baada ya mechi, Rodgers alisema, “Habari nzuri ni kuwa si jeraha la mguu. Tunatumai atakuwa sawa siku chache zijazo.
“Jamie ni mfumaji hodari wa mabao kwa timu yetu, ingawa tutapata mafanikio tu tukishirikiana kama timu.
“Hajatuchezea mechi kadha, ingawa timu imekuwa ikifanya vyema. Bila shaka tunataka awe katika hali nzuri. Yeye ni mchezaji mzuri sana na tunatumai si kitu kikubwa.”
Nne-bora
Leicester almaarufu Foxes imezoa alama 48 inapolenga kufuzu moja kwa moja kushiriki Klabu Bingwa Ulaya kwa kumaliza ligi ndani ya mduara wa nne-bora.
Vardy alistaafu kuchezea timu ya taifa ya Uingereza. Hata hivyo, ukatili wake mbele ya lango umezua madai kuwa kocha wa Uingereza Gareth Southgate huenda akajaribu kumshawishi abadili uamuzi huo kabla ya Kombe la Bara Ulaya (Euro 2020).
Southgate ameshuhudia washambuliaji wake Harry Kane na Marcus Rashford wakipata majeraha wiki chache zilizopita.