Starlets wapokelewa kibaridi JKIA licha ya ushindi
Na GEOFFREY ANENE
TIMU ya taifa ya soka ya wanawake ya Kenya imepata mapokezi baridi licha ya kupata ushindi muhimu wa mabao 3-0 dhidi ya wenyeji Zambia mjini Kitwe, Jumapili.
Hakuna kiongozi yeyote kutoka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) ama Wizara wa Michezo alikuwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta jijini Nairobi kupokea timu hiyo.
Hata hivyo, kikosi kizima cha Starlets wakiwemo makocha David Ouma na Richard Kanyi wamesema walijifunza mengi kutoka ziara ya Zambia na pia kupata motisha kubwa kabla ya kuanza kampeni ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AWCON) la mwaka 2018 nchini Ghana.
Katika mahojiano, Kanyi amesema, “Ushindi dhidi ya Zambia umetupa motisha kubwa. Pia umetusaidia kuona idara ambazo tuna nguvu ama ulegevu. Kurejea kwa Ouma kwenye benchi la kiufundi pia ni motisha kubwa tunapolenga kuwania tiketi ya kushiriki Kombe la Afrika kwa mara ya pili mfululizo. Mchuano huu pia umetuonyesha kwamba mshikamano unaendelea kuwa mzuri kikosini. Nimefurahishwa sana jinsi wachezaji watano wapya tuliowajumuisha walishirikiana vyema na wale wazoefu.”
Aidha, amesema kwamba anatumai mvamizi matata Esse Akida, ambaye alikosa mchuano wa Zambia kwa sababu ya anauguza jeraha, atakuwa amepona kabla ya Kenya kualika Uganda hapo Aprili 4.
“Licha ya kuwa tumekuwa tukipiga Uganda, tutachukulia mechi hiyo kwa uzito mkubwa kwa sababu hakuna timu ndogo siku hizi barani Afrika,” ameongeza na kumsifu Corazone Aquino, ambaye alipachika mabao mawili dhidi ya Zambia. “Kuwepo kwa Aquino kutoka kikosi cha wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 ni motisha kubwa. Ana nguvu na pia kasi nzuri,” amesema.
Ouma, ambaye aliongoza Starlets katika Kombe la Afrika mwaka 2016 nchini Cameroon, amefurahia kurejea kikosini baada ya kuwa nje muda mrefu.
Ameongeza, “Nimefurahishwa na mshikamano kati ya wachezaji wazoefu na wale wapya. Matokeo haya yameniridhisha.”
“Pia nafurahia kazi ambayo FKF imekuwa ikifanya kuhakikisha timu zote za taifa zinapiga mechi wakati wa kipindi cha mechi za kimataifa.
“Soka ya wanawake imeimarika. Naamini Uganda haijakuwa ikilala kwa hivyo tutatafuta kuzoa ushindi Uganda itakapozuru Kenya,” amesema.
Aquino amesema Starlets imejiandaa vyema tayari kukabiliana na Uganda. Mshambuliaji matata Mwanahalima Adam alitangulia kutikisa nyavu za Zambia katika kipindi cha kwanza kabla ya Aquino kuongeza mabao mawili katika kipindi cha pili.
Mshindi kati ya Kenya na Uganda baada ya mechi ya marudiano mnamo Aprili 8 atamenyana na mabingwa wa zamani Equatorial Guinea katika raundi ya pili. Mshindi wa raundi ya pili atafuzu kushiriki Kombe la Afrika nchini Ghana.