Straika Omala arejea kuibeba Gor baada ya Fifa kumpa kibali
MSHAMBULIZI wa Harambee Stars Benson Omala sasa anaweza kusakatia tena Gor Mahia baada ya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kumaliza mvutano baina yake na klabu ya Al Safa ya nchini Lebanon.
Omala hajakuwa akicheza kwa muda wa miezi minane na alirejea Gor Mahia mwezi Januari, lakini hangeweza kuchezea K’Ogalo kwa sababu uhamisho wake haukuwa umeidhinishwa na Fifa.
Al Safa — ambayo alijiunga nao mnamo Agosti 12, 2024 na kutia saini mkataba wa mwaka moja — walikuwa wamesisitiza kuwa bado alikuwa mchezaji wao.
Omala hakuwa amewachezea kwa sababu Ligi Kuu ya Lebanon ilisitishwa Septemba 25 mwaka jana kutokana na vita vilivyozuka kati ya wanamgambo wa Hezbollah nchini humo na taifa jirani la Israel.
Ligi hiyo ilirejelewa Januari 25 lakini Omala alikataa kurudi nchini humo akitaja sababu za kiusalama.
Lakini Al Safa nao walimkwamilia na wakishikilia alikuwa bado mwanasoka wao.
Utata kati ya Al Safa na Omala uliishia Fifa na juzi Jumatano mchezaji huyo alifahamishwa kuwa ameshinda mgogoro huo na sasa anaweza kuichezea K’Ogalo.
Kocha wa Gor Mahia, Sinisa Mihic, alifurahia habari hizo akisema kuwa sasa atakuwa akimtegea mshambulizi huyo matata kufungia K’Ogalo mabao katika mechi tisa walizosalia nazo kwenye Ligi Kuu (KPL).
“Nimefurahi kuwa hatimaye Omala yupo huru kutuchezea na utata uliokumba uhamisho wake sasa umekamilika. Ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga magoli na nitampanga kwenye mechi ya wikendi dhidi ya Bandari kwenye Kombe la Mozzartbet,” akasema Mihic.
Wakati wa debi ya Mashemeji mwezi uliopita, Mihic alikuwa amelalamkia kuwa hangeweza kumchezesha Omala ilhali ni mfungaji hodari ambaye anaweza kusaidia kuyainua matokeo ya klabu hiyo.
Mihic amemtaka Omala asahau masaibu ya kutocheza soka kwa miezi minane na amakinike kuimarisha kiwango chake, huku akieleza matumaini kuwa straika huyo atafanikiwa kucheza soka ya kulipwa nje ya nchi.
“Kwa sasa aimarishe kiwango chake na timu zitamwania. Aweke malengo fulani ya magoli; kutokana na ubora ambao ameonyesha awali, nina imani atawika,” akaongeza.
Wakati huo huo, Jopo la Kutatua Mizozo ya Spoti (SDT) imewaruhusu Dolphina Odhiambo na Sally Bolo kujumuishwa kwenye orodha ya wale ambao watashiriki kura za Gor Jumapili hii.
Pia SDT iliamrisha ada ya kushiriki kura hiyo ipunguzwe kutoka Sh500,000 hadi Sh150, 000 kisha naibu mwenyekiti alipe Sh125,000 kutoka Sh450,000.
Wanaomezea mate nafasi za katibu mkuu na mwekahazina watalipa Sh100,000 kutoka Sh400,000.