Michezo

Sum, Cherono na Chelimo kutumia mbio za Doha Diamond League na Kip Keino Classic kurejea katika ulingo wa Riadha

September 15th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

ZIKISALIA wiki tatu pekee kabla ya Riadha za Kip Keino Classic kuandaliwa katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, baadhi ya wanariadha wa haiba kubwa wa humu nchini wamefichua azma ya kunogesha kivumbi hicho cha Oktoba 3.

Kati ya watimkaji hao ni wale ambao kwa sasa wanajifua mjini Eldoret kwa minajili ya kushiriki duru ya nne ya Doha Diamond League nchini Qatar mnamo Septemba 25.

Kati ya fani zitakazovutia Wakenya katika riadha hizo za Doha ni mbio za mita 800 (wanawake na wanaume), mita 1,500 (wanawake na wanaume), mita 3,000 kuruka viunzi na maji (wanawake na wanaume) na mita 5,000 (wanawake na wanaume).

Kivumbi cha Kip Keino Classic kitatifuliwa siku moja kabla ya bingwa wa dunia na mshikilizi wa dunia Eliud Kipchoge kupimana ubabe na Mwethiopia Kenenisa Bekele katika mbio za London Marathon.

Wakenya wengine watakaonogesha London Marathon kwa upande wa wanawake ni Ruth Chepng’etich, Vivian Cheruiyot na mshikilizi wa rekodi ya dunia, Brigid Kosgei.

“Tumekuwa tukifanya mazoezi mazito licha ya kutokuwa na uhakika wa kushiriki mashindano yoyote hivi karibuni. Lakini mwishowe fursa imejipa kwa wanariadha wangu watatu – Eunice Sum (mita 800), Mercy Cherono (mita 5,000) na Margaret Chelimo,” akasema kocha Claudio Berardelli.

Mbali na watatu hao, Wakenya wengine wanaopigiwa upatu wa kutamba nchini Qatar wiki moja kabla ya kutifua kivumbi cha Kip Keino Classic ni bingwa wa dunia katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi Beatrice Chepkoech, bingwa wa dunia katika mbio za mita 1,500 Timothy Cheruiyot, malkia wa dunia katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri na bingwa wa Olimpiki katika mbio za mita 1,500 kwa upande wa wanawake, Faith Kipyegon.

Sum aliibuka bingwa wa dunia katika mbio za mita 800 mnamo 2013 jijini Moscow, Urusi huku Chelimo akiibuka mshindi wa nishani ya fedha katika Riadha za Dunia za 2019 zilizoandaliwa jijini Doha. Cherono ni bingwa wa zamani wa Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000.

Soufiane El Bakkali (Morocco), Marie-Josee Ta Lou (Ivory Coast), Lamecha Girma (Ethiopia) na Christian Taylor (Uingereza) ni miongoni mwa wanariadha wa haiba kuu kutoka mataifa ya nje ambao pia watanogesha Kip Keino Classic.

Kuwepo kwao kunatarajiwa kuibua msisimko zaidi miongoni mwa mashabiki 15,000 ambao Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) limetaka Wizara ya Afya na Wizara ya Michezo ziwape idhini ya kuhudhuria.

El Bakkali atatoana jasho na mfalme wa dunia na bingwa wa Olimpiki, Conseslus ‘Conse’ Kipruto kwenye mbio za mita 3,000 kuruka viunzi na vidimbwi vya maji. Conse alikosa duru mbili za ufunguzi wa mbio za Diamond League msimu huu jijini Monaco (Ufaransa), Stockhlom (Uswidi) na Brussels (Ubelgiji) baada ya kuugua Covid-19.

“Tumeanza mipango ya kupokea wageni watakaofanya mbio za Kip Keino Classic kuwa kivutio kikubwa. El Bakkali

atasafiri moja kwa moja hadi Nairobi baada ya kushiriki Diamond League jijini Doha,” akasema mkurugenzi wa mbio za Kip Keino Classic, Barnaba Korir.

“Kivumbi hiki kitakuwa na upekee mkubwa. Kitanogeshwa na wanamichezo maarufu zaidi ndani na nje ya bara la Afrika, akiwemo bingwa wa zamani wa dunia katika fani ya urushaji mkuki, Julius Yego,” akaongeza.

Ta Lou ambaye ni mwanamke mwenye kasi ya juu zaidi barani Afrika, atashiriki mbio za mita 100 na mita 200 kwenye Kip Keino Classic huku Taylor akitarajiwa kuwaamshia Wakenya ari ya kushiriki zaidi fani ya kuruka mara tatu.

Kip Keino Classic ni miongoni mwa duru za kivumbi cha World Athletics Continental Tour kilichofunguliwa rasmi nchini Finland mnamo Agosti 11, 2020.

Ingawa duru nzima imeitwa Kip Keino Classic kwa heshima ya mwanariadha veterani Kipchoge Keino, fani ya mbio za mita 10,000 wakati wa mashindano hayo kimeitwa “Naftali Temu 10,000m Classic.