• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Timu 40 kupigania taji la Tim Wanyonyi Super Cup

Timu 40 kupigania taji la Tim Wanyonyi Super Cup

Na JOHN KIMWERE

KIPANDE FC ni miongoni mwa zaidi ya timu 40 zinaoshiriki michezo ya kuwania taji la makala ya saba ya Tim Wanyonyi Super Cup.

Ngarambe hiyo hufadhiliwa na mbunge wa eneo la Westlands katika Kaunti ya Nairobi. Mchujo wa michuano ya taji hilo ambayo hushirikisha timu za wanaume na wanawake huandaliwa katika Wadi zote tano ikiwamo: Kangemi, Westlands, Karura, Moutain View na Kitisuru. Kangemi Wazoefu FC na Kangemi Ladies kutoka Wadi ya Kangemi ndio mabingwa watetezi kwa wanaume na wanawake mtawalia.

KUPAMBANA

Kipande FC ambayo hushiriki mechi za Ligi ya Kaunti iliyobanduliwa katika nusu fainali mwaka uliyopita raundi hii imeapa kupambana mwanzo mwisho kuhakikisha inabeba taji hilo. Wachana nyavu wa Kipande walimaliza tatu bora baada ya kuvuna mabao 2-1 mbele ya Leeds FC. ”Ninahisi nina timu nzuri ambayo imeonyesha ina uwezo wa kufanya kweli na kutwaa taji la mwaka huu,” kocha wa Kipande, Pasafa Sama na kuongeza kuwa anafahamu haitakuwa shughuli rahisi.

Kocha huyo anadokeza kuwa kiasi wachezaji wengi wamepoteza makali yao dimbani baada ya kukawia muda mrefu bila kushiriki mechi zozote hali iliyochangiwa na janga la corona lililotua nchini mwezi Machi 2020. Kwenye mechi ya ufunguzi Kipande FC chini ya nahodha, Martin Kimathi ilizima Kakamega Homeboyz kwa magoli 5-0 Uwanjani City Park, Nairobi. Nahodha huyo anakiri kwamba wamepania kujituma kwa udi na uvumba angalau kufanya kweli kwa kushinda mechi zote zinazopigwa kwa mtindo wa muondoano.

Naye kocha wa Mshikemshike, Allan Shibega anasema ”Bila shaka nimeteua wachezaji wale bora katika kikosi changu jambo linalonipa imani kuwa tumekaa vizuri kushinda taji hilo.”

Kwenye makala ya kipute hicho mwaka uliyopita timu hiyo ilibanduliwa katika hatua za robo fainali. Hata hivyo anadokeza kuwa mashindano ya mwaka huu hakuna mteremko maana suala la mlipuko wa corona limedidimiza mchezo wa vijana wengi.

Kocha wa Slum Dwellers, Shabana Masika akiongea na vijana wake. Picha/John Kimwere

MATENDO MAOVU

Kadhalika alitia shaka hatua ya Kangemi Wazoefu kufanya kweli huku akishikilia kuwa imepoteza baadhi ya wachezaji waliohamia Kangemi Allstars.

Ujio wa kinyang’anyiro hicho ni afueni kubwa kwa wachezaji ambao ni wanafunzi ambao hawamo shuleni. Mwakilishi wa vijana katika Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Tawi la Nairobi Magharibi, Hannington Kimathi anasema mechi hizo zinafanya vijana wamakinike viwanjani na kujiepusha matendo maovu mitaani.

Katika mpango mzima mechi za mchujo kwa mtindo wa muondoano zinapigwa katika kila Wadi ambapo timu mbili zitajikatia tiketi ya kushiriki mechi za robo fainali.

Wapenzi wa soka wakifuatilia mechi mojawapo ya mashindano ya kuwania taji la Tim Wanyonyi Super Cup uwanjani Kihumbu-ini, Kangemi. Picha/John Kimwere

BAADHI YA MATOKEO

Kwa timu za wanawake Kipande Ladies iliandikisha ufanisi wa pointi tisa na kusonga mbele kwenye mechi za Wadi ya Karura. Katika mechi za Wadi ya Kangemi, wachezaji wa Patriots Queens walipiga Real Starlets magoli 6-0 huku Kangemi Ladies wakivuna mabao 5-1 mbele ya Waruku Sportiff.

Vipusa wa Kipande Ladies walitembeza soka la kuvutia na kufanikiwa kunyamazisha Runda View, RYSA Ladies na Gachie Ladies. Kwa jumla warembo hao wa Kipande walivuna mabao 29-0 katika mechi hizo tatu. ”Bila shaka nashukuru wachezaji wangu kwa kazi nzuri wameonyesha wamepania kubeba taji la muhula huu,” kocha huyo alisema.

Kangemi Ladies iliteremsha soka safi na kuzima ndoto ya wenzao kutokana na juhudi zake Irene Anyango mabao mawili nao Salome Drailer, Vallary Clara na Joan Makobe kila mmoja alitupia kambani goli moja. ”Ushindi huo umetuweka pazuri kusonga mbele lakini tutahitaji kushinda mechi sijazo,” kocha wa Kangemi Ladies, Loice Karanja alisema. Nao vigoli wa Patriots Queens walilemea wapinzani wao na kupata mabao hayo kupitia Peris Akinyi ‘Hat trick,’ Joy Lubadiri aliyetikisa nyavu mara mbili huku Faith Nyakiri akipiga kombora moja.

Timu ya Slum Dwellers. Picha/John Kimwere

 

You can share this post!

Wakenya Jeptoo na Kotut wasikitika baada ya mbio za Paris...

Anatumia mitandao ya kijamii kuhamasisha umma kuhusu Ukimwi