Michezo

Timu za magongo zilivyotamba licha ya kukosa hela

January 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

MWAKA uliyopita Kenya ilijikuta pagumu katika magongo baada ya umaskini kuchangia timu za wanaume na wanawake kukosekana kwenye shindano la Klabu Bingwa Afrika (CCCA) lililoandaliwa nchini Misri.

Kwa mara ya kwanza Kenya ilishindwa kushiriki ngarambe hiyo hasa baada ta Kampuni ya Telkom kuacha kufadhili kikosi cha wanawake cha Blazers (awali Telkom Orange). Kwa jumla Telkom Orange na Scorpions ya Chuo cha Strathmore zilikuwa ziwakilishe Kenya katika pambano hilo.

Msoto unaotesa sekta ya spoti hapa Kenya ulikatiza mpango wa madume wa Butali Warriors na Kenya police kutoshiriki ngarambe hiyo.

Hata hivyo wanamagongo wa vikosi hivyo walionyesha vita vya ubabe kwenye mbio za Ligi Kuu ya wanaume na wanawake.

Aidha makambiliano ya kiana yalishuhudiwa kwenye michezo ya kuwania mataji hayo ya Supa Ligi kwa wanaume na wanawake.

Hatua ya chama cha kitaifa cha hoki (KHU) kuanzisha ligi hiyo muhula huo ulifanya idadi kubwa ya timu za magongo kushiriki kampeni za msimu huo.

Parkroad Badgers na Mombasa Sports Club kila moja itashiriki Ligi Kuu msimu huu baada ya kuibuka kati ya nafasi mbili za kwanza kwa alama 51 na 43 mtawalia.

Kiukweli timu za wanawake zilizoshiriki ngarambe hiyo kamwe hazikulaza damu. Timu ya DFG Wolverines ya kocha, Gordon Odwuor ilishusha mechi za kusisimua na kubeba ubingwa huo kwa kuvuna pointi 32, mbele ya Oranje Leonas.

Matokeo hayo yalisaidia vikosi hivyo kunasa tiketi za kushiriki Ligi Kuu muhula ujao. ”Nashukuru Mungu kwa kuwapa wachezaji wangu nguvu na maarifa kwenye kampeni zetu walikotenda kweli na kusonga mbeke,” anasema kocha huyo.

Aliongeza kuwa kinyang’anyiro cha Ligi Kuu msimu mpya kinatazamiwa kuwacha moto mkali. ”Itakuwa mwanzo kwetu kushiriki Ligi Kuu lakini hatutashiriki kusukuma wengine mbali tutakuwa kwa mashindano tukilenga kubeba taji hilo,” asema.

Vipusa wa Blazers ya kocha, Jos Openda wamekomaa katika kampeni za kipute hicho baada ya kubeba kombe hilo mara 22.

Naye kocha wa Orange Leonas, David Omwaka anasema ”Bila shaka mechi za Ligi Kuu muhula mpya zinapigiwa chapuo kuonekana kivingine tofauti na misimu iliyopita.”

Nao madume wa Jomo Kenyatta (JKUAT) walitwaa ubingwa wa Ligi ya Taifa. JKUAT iliibuka ya kwanza kwa alama 28, nne mbele ya Parkroad Tigers na zote kujikatia tiketi ya kupanda ngazi ngarambe ya Supa Ligi.

Wanamagongo watano walioibuka mashujaa kwa kuzipiga jeki pakubwa timu zao kwenye kampeni za Ligi hizo kila mmoja alitwaa tuzo ya mchezaji anayeimarika (MVP).

Wanaume- Ligi Kuu:Festus Onyango (Strathmore University), Supa Ligi:Moses Obushuru(TUK) na Ligi ya Taifa: Christian Kwama.

Wanawake-Ligi Kuu:Beatrice Mbugua (USIU-A) na Supa Ligi:Pauline Ochieng Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN).