Tuko tayari kukabiliana na Gambia, asema kocha Beldine Odemba
KOCHA wa Harambee Starlets, Beldine Odemba amekiri kuwa, timu yake iko tayari kwa mechi ya leo dhidi ya Gambia katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2026.
Mchezo huo utachezwa katika uwanja wa Stade Lat Dior uliopo mjini Thies, Senegal, saa kumi jioni saa za Senegal, (saa moja usiku kwa saa za Kenya).
Kuelekea mechi hiyo, Kenya inahitaji kuepuka kufungwa kwa zaidi ya mabao mawili ili kusonga mbele. Sare itahakikisha kufuzu kwao kama mshindi wa jumla ya mabao.
Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Nairobi Ijumaa iliyopita, Starlets waliwashinda Gambia, wanaojulikana kama The Scorpion, 3-1 katika uwanja wa Nyayo National jijini Nairobi.
Washambuliaji Mwahalima Adam, Fasilah Adhiambo, na Sheylene Opisa walifungia Kenya katika dakika ya 12, 19, na dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza, mtawalia.
Nahodha na mshambuliaji Fatuomata Kanteh wa Gambia alifunga bao la ufunguzi kwa Gambia katika dakika ya pili.
Akizungumza Jumatatu wakati wa mazoezi yao ya mwisho huko Thies, Odemba alisema, “Wasichana wako tayari na wana morali ya juu, wakijua kuwa kazi bado haijakamilika. Wana hamu ya kucheza katika majukwaa makubwa kama WAFCON.”
Odemba, mwenye leseni ya ukocha ya A, aliongeza, “Tunataka kuandika historia, haswa baada ya miaka 10 ya kujaribu kurejea WAFCON. Kufuzu kutathibitisha ukuaji mkubwa katika soka la wanawake nchini na kuunda fursa kwa wachezaji wetu kujiunga na vilabu vya juu nje ya nchi.”
Kufuzu kutaashiria kuonekana kwao kwa mara ya pili kwenye mashindano katika muongo mmoja, kufuatia majaribio yaliyoshindwa mnamo 2018, 2022, na 2024 bila mafanikio.
Odemba, akiungwa mkono na manahodha Ruth Ingosi na Dorcas Shikobe, aliwahimiza mashabiki wa Kenya nchini Senegal kujitokeza kuwapa sapoti na wale walioko nyumbani kuwashabikia.
Shikobe aliongeza, “Tuko tayari kufuzu tena na itakuwa fursa nzuri. Kwa mashabiki wa Kenya nchini Senegal, njooni mtushangilie na kwa Wakenya walioko nyumbani, najua mnatupenda, na sisi tunawapenda pia.”
Shikobe, pamoja na viungo Corazone Aquino na kipa Lilian, walikuwa sehemu ya kikosi cha 2016 kilichofuzu WAFCON chini ya kocha wa zamani David Ouma. Adam na beki Enez Mango walicheza kwenye mechi za kufuzu lakini hawakujumuishwa kwenye kikosi cha mwisho.
Ingosi alisema, “Morali iko juu tangu mechi ya kwanza, na tutaendelea na morale hiyo hiyo. Tuko hapa kuandika historia. Hatutawaangusha. Gambia wamekuwa wakiongea, lakini tunawaheshimu lakini tutapambana uwanjani.”
Huendxa Odemba akamwanzisha Awuor langoni, Lorine Ilavonga, nahodha Ingosi na Mango kwenye safu ya ulinzi. Elizabeth Muteshi, Lavender Akinyi, Martha Amnyolete na Adhiambo wakidhibiti eneo la kati huku Elizabeth Wambui, Opisa, na Adam wakishambulia.