Michezo

TUKUTANE KASARANI: Mastaa wa Everton wafika Nairobi kushuhudia mchuano wa The Toffeemen dhidi ya Kariobangi Sharks

July 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MASHUJAA wa zamani wa klabu ya Everton, Steven Pienaar kutoka Afrika Kusini na Mwingereza Leon Osman wako nchini tayari kwa mechi ya kimataifa kati ya mabingwa wa soka ya SportPesa Super Cup Kariobangi Sharks na washindi mara tano wa Kombe la FA, Everton.

Timu hizi zitakutana uwanjani Kasarani mnamo Julai 7 katika makala haya ya tatu.

Pienaar na Osman sasa ni mabalozi wa Everton baada ya kustaafu wakiwa wameichezea mechi 189 na 433, mtawalia. Waliwasili nchini Kenya mnamo Jumatano kama sehemu ya maandalizi ya mchuano huo wa kirafiki unaosubiriwa kwa hamu kubwa.

Vijana wa Kocha Marco Silva wanatarajiwa kuwasili jijini Nairobi mapema Jumamosi. Ziara hiyo itakuwa ya kwanza kabisa ya Everton nchini Kenya, lakini ya pili katika eneo la Afrika Mashariki baada ya kuzuru Tanzania mwaka 2017 kupepetana na miamba wa Kenya, Gor Mahia katika makala ya kwanza.

Staa wa zamani wa klabu ya Everton, Steven Pienaar wa kutoka Afrika Kusini (mwenye mkono mmoja mfukoni) akiwa jijini Nairobi, Ijumaa, Julai 5, 2019. Picha/ Hisani

Everton ilishinda mchuano huo 2-1 jijini Dar es Salaam na kunyoa Gor bila maji 4-0 ilipoialika uwanjani Goodison Park nchini Uingereza kwa makala ya pili mwaka 2018.

Mkuu wa masuala ya usalama kutoka kwa wadhamini, kampuni ya SportPesa, Matthews Waria, amehakikishia mashabiki usalama wa kutosha. Amesema Alhamisi, “Tuko tayari. Kujeni uwanjani na mfurahie mechi.”

Naye Afisa Mkuu wa Mauzo wa SportPesa Kelvin Twissa amesema, “Nairobi iko tayari kwa soka ya kiwango cha dunia.”

Tiketi za kawaida zinapatikana kwa Sh100 katika maeneo yafuatayo:

680 Hotel

New Stanley

City Market

Tuskys Beba Beba

Kencom City Hall Way

Jevanjee

Moi Avenue karibu na Ambassador

Haile Selassie – eneo la Bomb Blast

Kenyatta Avenue – GPO

Kenya Cinema – Moi Avenue

Galitos – Kenya Towers

Uchumi – Aga Khan Walk

Kimathi Street – Nanak House

TRM