Tunisia yazamisha Ghana na kujikatia tiketi ya nane-bora
Na MASHIRIKA
ISMAILIA, MISRI
TUNISIA waliwapepeta Ghana 5-4 kupitia mikwaju ya penalti na hivyo kufuzu kwa hatua ya robo-fainali itakayowakutanisha na Madagascar kwenye makala ya 32 ya Kombe la Afrika (AFCON) nchini Misri.
Kipa Farouk Ben Mustapha aliwabeba Tunisia katika mchuano huo baada ya kutoka benchi mwishoni mwa kipindi cha ziada kwa lengo la kuzidaka penalti za wapinzani, na kwa kweli akafaulu kuupangua mkwaju wa Caleb Ekuban.
Awali, Tunisia walikuwa pua na mdomo kuibuka washindi wa mchuano huo katika muda wa kawaida kwa bao 1-0.
Ingawa hivyo, beki Rami Bedoui aliyetokea benchi mwishoni mwa kipindi cha pili, alijifunga katika dakika ya 90 na kurejesha Black Stars ya Ghana mchezoni.
Tunisia ambao waliibuka mabingwa wa fainali za AFCON walizoziandaa mnamo 2004, walijipa uongozi katika dakika ya 73 kupitia kwa Taha Yassine Khenissi aliyekamilisha krosi ya Wajdi Kechrida kwa ustadi mkubwa.
Ekuban ambaye ni mvamizi wa Leeds United nchini Uingereza, ndiye mchezaji wa pekee aliyepoteza penalti kwa upande wa kikosi cha Ghana ambacho kilizamishwa zaidi na Ferjani Sassi aliyewachanjia Tunisia mkwaju wa mwisho.
Tunisia almaarufu ‘The Carthage Eagles’ kwa sasa wamepangiwa kuchuana na Madagascar ambao ni wa 108 duniani katika robo-fainali itakayowakutanisha mjini Ismailia mnamo Alhamisi.
Kikosi hicho kilifuzu kwa hatua ya 16-bora baada ya kusajili sare tatu katika michuano yote ya Kundi E lililowajumuisha pia Mali, Angola na Mauritania.
Licha ya Ghana kutamalaki mchezo na kuonekana kuwazidi Tunisia maarifa katika takriban kila idara, juhudi zao zilishindwa kabisa kuzalisha matunda yoyote huku fowadi Nuhu Kasim akishuhudia kombora lake katika dakika ya 34 likibusu mwamba wa goli la wapinzani.
Ingawa ushirikiano mkubwa kati ya Thomas Partey na Jordan Ayew ulichangia bao lililopachikwa wavuni na nahodha Andre Ayew, refa alikataa kulihesabu goli hilo la dakika ya 66 kwa madai kwamba Partey alikuwa ameunawa mpira kabla ya Andre kuujaza kimiani.
Hata hivyo, marejeleo ya picha za video yalionyesha kwamba Partey aliudhibiti mpira huo kwa kifua badala ya mkono kama alivyodai refa baada ya kushauriana na msaidizi wake.
Tunisia yadhibiti mchezo
Tunisia walianza kudhibiti mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira kunako dakika ya 68 baada ya Wahbi Khazri aliyekuwa akiuguza jeraha kutokea benchi na kuingia ugani. Dakika chache baadaye, krosi yake ilifumwa wavuni na Khenissi.
Ushindi wa Tunisia katika mchuano huo unamaanisha kwamba Ghana wanakosa kutinga nusu-fainali za AFCON kwa mara ya kwanza tangu 2008. Isitoshe, ilikuwa ni mara ya kwanza kwa Tunisia kusajili ushindi dhidi ya Ghana katika historia ya kushiriki kwao fainali za AFCON.
Ilikuwa ni mara ya tatu kwa Ghana kubanduliwa kwenye kampeni muhimu za kimataifa kupitia mikwaju ya penalti. Kikosi hicho kilikosa fursa ya kuweka historia ya kuwa timu ya kwanza ya Afrika kuwahi kutinga robo-fainali za Kombe la Dunia mnamo 2010 baada ya mvamizi Asamoah Gyan kupoteza penalti dhidi ya Uruguay nchini Afrika Kusini. Aidha, kikosi hicho kilizidiwa maarifa na Ivory Coast kwenye fainali ya AFCON iliyowakutanisha nchini Equatoria Guinea mnamo 2015.
Kadhia ya Tunisia katika fainali za AFCON hadi kufikia sasa inawiana na ya Benin ambao kwa sasa wanajiandaa kuchuana na Senegal kwenye robo-fainali licha ya kutosajili ushindi wowote katika hatua ya makundi.