• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 4:55 PM
Tutawaandalia kura ya kufana FKF – bodi mpya

Tutawaandalia kura ya kufana FKF – bodi mpya

Na GEOFFREY ANENE

MWENYEKITI mpya wa Bodi ya Uchaguzi wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), Kentice Tikolo ameahidi kuwa wataendesha shughuli hiyo kwa njia ya kufana.

Akizungumza baada ya FKF kuzindua rasmi bodi hiyo ya maafisa wanane jijini Nairobi hapo Jumatatu, Tikolo alihakikishia Wakenya kuwa uchaguzi utafanyika katika muda uliowekwa na Shirikisho la Soka Dunia (FIFA), wa Machi 30, 2020.

Fifa imepatia Kenya makataa hayo ya siku 60 kuchagua maafisa wapya wa shirikisho, kwa sababu imechelewa kufanya hivyo.

“Kuzinduliwa rasmi kwa bodi hii leo (jana Jumatatu) kunamaanisha kuwa kazi ya uchaguzi inaanza rasmi leo. Kitu cha kwanza ambacho tutafanya kama bodi ni kwamba, kufikia Februari 7 tutakuwa tumetoa ratiba ya uchaguzi wa maafisa wa kaunti kwanza, halafu upishe ule wa kitaifa.

Uchaguzi tutakaoandaa utakuwa mfano kwa mashirika yanayoendesha uchaguzi humu nchini. Hatutapendelea yeyote,” alisema mtaalamu huyo wa mawasiliano, ambaye pia ni mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Wazito FC.

Tikolo atasaidiwa na Patrick Onyango, ambaye ni mshauri wa masuala ya kuendesha michezo katika Fifa. Onyango atahudumu kama Katibu.

Mwanahabari Ali Hassan Kauleni, refa wa zamani Alfred Ndinya pamoja na Samuel Karanja, Rachel Muthoga, Elaine Mbugua na Andrew Mudibo watakuwa wanachama.

Bodi hiyo ni mpya kabisa baada ya ile iliyoongozwa na Profesa Edwin Wamukoya kutupiliwa mbali kufuatia utata uliosababisha uchaguzi huu, uliopangiwa kufanyika Desemba 7, 2019, kufutiliwa mbali Novemba 15 iliyofuata.

Eunice Lumallas (Katibu), Abdi Said, Robert Nyakundi na Elynah Shiveka walihudumu katika bodi iliyopita. Ilikuwa imeandaa uchaguzi wa mashinani na kaunti kabla ya Msajili wa Vyama vya Michezo kuifutilia mbali kwa kwenda kinyume na sheria za michezo za 2013.

Wakati huo huo, Afisa Mkuu Mtendaji wa FKF, Barry Otieno jana alieleza sababu zilizofanya mkutano kati ya Waziri wa Michezo Amina Mohamed, Rais wa FKF Nick Mwendwa, Mahakama ya Kusikiza Kesi za Michezo (SDT), Msajili wa Vyama vya Michezo na maafisa wa FIFA kukosa kufanyika.

“Hakukuwa na haja twende mjini Zurich, Uswizi kukutana na Fifa baada ya sisi wenyewe kuelewana kuwa FKF itafanya uchaguzi, halafu tuendelee kutimiza masharti ya sheria za 2013 polepole.

“Si rahisi kutimizwa mara moja, gharama yake ni kali. Kuna klabu 6,000 za soka nchini Kenya, ambazo FKF itagharimika kuandikisha wachezaji kwenye rejesta ya Msajili wa Vyema vya Michezo nchini,” alisema Otieno akizindua bodi hiyo mpya katika makao makuu ya FKF mtaani Kasarani jana Jumatatu.

Majukumu ya bodi hiyo, ambayo imetengewa afisi katika makao makuu ya FKF, ni kuendesha uchaguzi kutoka kaunti hadi kitaifa, kuandaa uchaguzi na pia itasikiza rufaa.

Bodi hiyo tayari ina kibarua kigumu cha kuridhisha kila mtu. Kuna viongozi wengine wa zamani kama aliyekuwa mwenyekiti wa shirikisho la soka nchini Sam Nyamweya, ambao wamedai kuwa baadhi ya maafisa kwenye bodi mpya ni marafiki wa Mwendwa anayetetea wadhifa wake.

You can share this post!

Taifa laendelea kuomboleza vifo vya wanafunzi 14 Kakamega

Miereka ya Uhuru na Ruto yamwinua Raila kisiasa

adminleo