Michezo

Uganda, Burundi wavuna ushindi Cecafa U20 ikipamba moto

September 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Uganda wamechupa uongozini mwa Kundi A kwenye mashindano ya soka ya Afrika Mashariki na Kati ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 20 baada ya kulipua Djibouti 5-1 mjini Gulu, Jumatatu.

Uganda, ambayo ilitolewa kamasi dhidi ya Eritrea katika mechi yake ya ufunguzi iliyotamatika 1-1 Septemba 21, ilirejea uwanjani Pece kwa kishindo na kupepeta Djibouti kupitia mabao ya Steven Sserwadda dakika ya 25 na 52, Ivan Bogere (43), Isma Mugulusi (82) na Justine Opiro (86). Kalid Osman Elmi alifungia Djibouti bao la kufutia machozi dakika ya 53.

Sudan, ambayo ilichapa Djibouti 4-0 katika mechi ya kundi hili iliyokuwa ya kufungua mashindano, imekabwa 3-3 dhidi ya Eritrea, Jumatatu. Eritrea ilifungua ukurasa wa mabao kupitia kwa Mewael Tesfai Yosief dakika ya 10. Sudan ilijibu na mabao mawili kutoka kwa Mohamed Abbas Namir dakika ya 40 na Shihab Eldeen Siddiq Abdalrahman kabla tu ya mapumziko.

Hata hivyo, Eritrea ilijikakamua katika kipindi cha pili na kusawazisha 2-2 kupitia kwa penalti ya Robel Teklem Michael dakika ya 55 na kisha ikachukua uongozi kupitia kwa Ali Suleiman Ibrahim dakika ya 72. Ilipokonywa na Sudan ushindi kinywani Musab Kurdman Elfaki alipofanya mabao kuwa 3-3 kupitia penalti katika dakika za majeruhi.

Burundi ilizaba Somalia 2-1 kupitia wachezaji Hakizimana Hamimu dakika ya 40 na Louis Romeo Ndunimana dakika ya 56 nayo Somalia ikajiliwaza na bao kutoka kwa Ahmed Abdullahi Abdi kabla ya kipenga cha mwisho kulia.

Burundi imekamilisha mechi zake za Kundi C linalojumuisha mataifa matatu. Iliambulia alama moja katika mechi yake ya ufunguzi ilipotoka 3-3 dhidi ya Sudan Kusini uwanjani Njeru.

Kenya ya kocha Stanley Okumbi iko katika Kundi B pamoja na Ethiopia, Zanzibar na Tanzania. Vijana wa Okumbi walipepeta Zanzibar 5-0 nayo Tanzania ikalima Ethiopia 4-0 katika mechi zao za ufunguzi. Kenya na Tanzania zitagaragarazana Septemba 24.

Timu tatu za kwanza kutoka makundi A na B pamoja na mbili bora kutoka Kundi C zitaendelea na mashindano hapo Septemba 29 na Septemba 30, ambazo ni tarehe za mechi za robo-fainali. Nusu-fainali ni Oktoba 2 halafu fainali ni Oktoba 5.