Ugomvi wa Gor na AFC Mashemeji Derby ikija
AFC Leopards na Gor Mahia zinaendelea kuimarisha maandalizi yao kwa Debi ya Mashemeji huku taharuki ikianza kuchipuka kuhusiana na kipute hicho cha Jumapili, Machi 30, 2025.
Mchuano huo mkubwa zaidi wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) unatarajiwa kusakatwa katika uga wa Nyayo ambao una uwezo wa kuwasitiri mashabiki 22,000.
Siasa na shinikizo za mashabiki zimechangia taharuki kuanza kupanda kabla ya debi hiyo kati ya mahasimu hao wa tangu jadi.
Katika mizani ya kisiasa, kupigwa kwa Mbunge wa Mumias Mashariki Peter Salasya na wahuni aliodai wanatoka jamii fulani kumechipuza vita vya kisasi kutoka kwa mashabiki wa Ingwe.
Salasya ambaye alikuwa amevalia jezi ya Ingwe alipigwa na kufurushwa nje ya uwanja wakati ambapo Kenya ilikuwa ikichuana na Gabon.
Mitandaoni kumekuwa na majibizano makali kati ya mashabiki wa Ingwe na K’Ogalo kuhusu tukio hilo.
Wale wa Leopards wamesisitiza kuwa Salasya lazima aje Nyayo na wako tayari kwa kisasi huku wenzao wa Gor wakiapa kuwa hawatamruhusu mwanasiasa huyo kutia guu Nyayo na wako tayari kumwadhibu.
Mashabiki wa Gor wanamwaandama Salasya kutokana na kejeli na matusi ambayo amekuwa akiyaelekeza kwa Kinara wa upinzani Raila Odinga.
Binafsi amesema atakuwa Nyayo kwa debi hiyo.
Majibizano kati ya mashabiki hao yanajiri wakati ambapo Mwenyekiti wa Kamati Andalizi ya dimba la Mataifa Bingwa Afrika (CHAN) Nicholas Musonye, ameonya kuwa timu hizo mbili hazitacheza Nyayo au Kasarani iwapo fujo zitatokea Jumapili na waharibu viti Nyayo.
“Tunawaomba mashabiki wetu wawe na amani na wafurahie mchezo bila kujali matokeo kisha waende nyumbani. Si vyema kuchanganya soka na siasa na sisi kama Gor tunawaomba mashabiki wetu wazingatie amani,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Ray Oruo.
Maafisa wa timu hizo mbili wanatarajiwa kuandaa mkutano na wanahabari mnamo Ijumaa ambapo watazungumzia mikakati ya kiusalama kuelekea mtanange huo.
Uwanjani, makocha wa Gor na Leopards Sinisa Mihic na Fred Ambani watakuwa na shinikizo kila mmoja akitaka kushinda mchuano huo.
Mashabiki wa Gor tayari wamemwaambia Mihic ajiandae kufunganya virago na kurejea Croatia kama watapoteza kwa Leopards.
Kwenye mechi tano, ambazo amesimamia, ameshinda tatu na kutoka sare mbili.
Kocha wa Ingwe Fred Ambani naye anamulikwa kwa sababu Ingwe haijakuwa ikiyapata matokeo ya kuridhisha uwanjani.