Michezo

Ulinzi Stars yaanza michezo ya wanajeshi ya Afrika Mashariki kwa kumiminia Burundi mabao 4-0

August 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

WENYEJI Ulinzi Stars wameanza kampeni ya kutetea taji la soka kwenye michezo ya wanajeshi ya Muungano wa Afrika Mashiriki (EAC) kwa kishindo baada ya kuchabanga Burundi 4-0 mnamo Jumanne katika uwanja wa kimataifa wa Kasarani jijini Nairobi.

Mabingwa hawa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mwaka 2003, 2004, 2005 na 2010 walipata mabao hayo muhimu kutoka kwa washambuliaji Oscar Wamalwa (matatu) na Enosh Ochieng’.

Wamalwa alitikisa nyavu za Burundi katika dakika ya saba na kuimarisha uongozi huo katika dakika ya 57.

Mfungaji bora wa KPL msimu 2018-2019 Ochieng’, ambaye aliingia kama mchezaji wa akiba katika kipindi cha pili, alifuma wavuni bao la tatu dakika ya 76 kabla ya Wamalwa kupata ‘hat-trick’ yake dakika mbili baadaye.

Ulinzi inatumia mashindano haya kujiandalia msimu mpya wa 2019-2020 wa KPL utakaoanza Agosti 30. Mechi ya ufunguzi ya Ulinzi itakuwa ugenini dhidi ya washiriki wapya Kisumu All Stars mnamo Agosti 31.

Kikosi cha Ulinzi Stars: Wachezaji 11 wa kwanza – Timothy Odhiambo (kipa), Brian Birgen, Omar Mbongi, Bonventure Muchika, Hassan Mohamed, Okinyi, Daniel Waweru, Churchill Muloma, Oscar Wamalwa, Elvis Nandwa, Omar Boraafya. Wachezaji wa akiba – James Saruni (kipa), Boniface Andayi, Hamisi Abdalla, Enosh Ochieng’, Ibrahim Shambi, Ali Swaleh, Bernard Ongoma.

Ratiba ya soka

Agosti 13

Kenya 2-0 Burundi

Agosti 14

Uganda na Rwanda

Agosti 15

Tanzania na Burundi

Agosti 16

Kenya na Uganda

Agosti 17

Rwanda na Burundi

Agosti 19

Tanzania na Kenya

Agosti 20

Burundi na Uganda

Rwanda na Tanzania

Agosti 22

Uganda na Tanzania

Agosti 23

Rwanda na Kenya