Umaru Kasumba aibuka mchezaji bora wa KPL Aprili
Na GEOFFREY ANENE
MGANDA Umaru Kasumba ndiye mchezaji bora wa tuzo ya Waandishi wa Habari za Michezo wa Kenya (SJAK) wa mwezi Aprili.
Mshambuliaji huyu kutoka klabu ya Sofapaka aliwashinda Whyvonne Isuza (AFC Leopards), Enosh Ochieng’ (Ulinzi Stars) na Allan Wanga (Kakamega Homeboyz).
Kasumba alizoa kura 23 dhidi ya Isuza, Wanga na Ochieng’ waliopata 21, 16 na 10 mtawalia.
Mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 25 alitetemesha sana mwezi Aprili alipofungia waajiri wake mabao saba ligini wakifukuza viongozi Gor Mahia.
Alipachika mabao mawili Sofapaka ikirarua Zoo mjini Kericho na pia kupata idadi sawa katika sare ya 2-2 dhidi ya Mathare United.
Kasumba alifunga bao lililozamisha KCB 1-0, akaona lango Sofapaka ikitoka 1-1 dhidi ya Kariobangi Sharks na kujaza wavuni bao la pekee ikichapa SoNy Sugar 1-0.
Amepata tuzo hii mara mbili msimu huu wa 2018-2019. Aliibuka mshindi mwezi Februari.
Wachezaji wengine walioshinda taji hili msimu huu ni Peter Thiong’o (Homeboyz) mwezi Desemba, Abdallah Hassan (Bandari) mwezi Januari na Justin Ndikumana (Sofapaka) mwezi Machi.
Wanga, Kasumba na Ochieng’ wanashikilia nafasi tatu za kwanza kwenye vita vya kutwaa tuzo ya mfungaji bora ligini msimu huu baada ya kucheka na nyavu mara 18, 17 na 16 mtawalia.