Uongozi wa Gor watetea uteuzi wa Mihic
WAKATI ambapo Kocha Sinisa Mihic anaendelea kuanza maisha ndani ya klabu Gor Mahia, maswali yameibuka jinsi ambavyo uongozi wa klabu uliamua kumpa kazi hiyo.
Mihic, 48 alitambulishwa rasmi kama kocha wa Gor Mahia mnamo Jumatatu asubuhi na sasa anakabiliwa na kibarua cha kuhakikisha wanashinda ubingwa wa Ligi Kuu (KPL) kwa mara ya 22.
Mnamo Jumatatu, Mwenyekiti wa Gor Ambrose Rachier alisema raia huyo wa Croatia amepewa mkataba wa miezi sita na utaongezwa tu iwapo ataridhisha uongozi wa klabu.
Rachier alisema kocha mpya anafahamu matukio ya baadhi ya makocha wa kigeni klabuni humo wamepitia lakini akakubali kuongoza timu hiyo ishinde mechi zake.
Leonardo Neiva, raia wa kigeni kuifunza Gor alitimuliwa na mashabiki wa klabu kutokana na matokeo mabaya, wakati mwingine baadhi hata wakimpiga. Je Mihic atavumilia pandashuka za KÓgalo timu ikikosa kufanya vizuri?
“Neiva alianza kukosana na wachezaji na wakaungana kumpinga. Kazi ambayo kocha wetu atafanya kwa miezi sita itaamua iwapo tutamwongezea kandarasi au la,” akasema Rachier.
Mtihani wa kwanza kwa Mihic ni Jumamosi hii ambapo K’Ogalo itavaana na Mathare United kwenye uga wa Dandora, Nairobi.
Hata hivyo, maswali yameibuka jinsi KÓgalo waliamua kutwaa huduma za kocha huyo ilhali hajakuwa kazini kwa miaka miwili. Mara ya mwisho alifanya kazi ni kwa mabingwa mara nne wa Ligi Kuu ya Kuwaita Al-Samiya mnamo 2022.
Alihudumu kama naibu kocha kwa siku 16 kati ya Februari 12-Februari 28. Awali alikuwa amezifunza NK Crikvenica , Al Shabaab na Al-Fahaheel ambazo zinashiriki ligi ya Croatia.
Kwenye taaluma yake ambayo ni zaidi ya miaka 25 amekuwa kocha wa Al-Ahli Saudi Arabia. Kama naibu kocha alihudumu kama kocha wa Al-Nasr SC ya Libya na Al Merrikh ya Sudan.
Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Ray Oruo jana alisema kocha mpya anastahili kupewa muda wa kuchapa kazi badala ya kumakinikia jinsi ambavyo aliteuliwa.
“Yeye ni kocha mwenye uzoefu na tulimteua kutoka kwa orodha ya makocha 40 waliotuma maombi yao. Kile ambacho atakifanya ndiyo muhimu badala ya kumakinikia jinsi ambavyo alipata kazi,” akasema Oruo.
“Siwezi kufichua katika orodha hiyo na alipata alama za juu au za chini na kwa nini huyu ama yule hakupewa ila kama klabu tuliafikiana na kumpa kazi kwa sababu tuna imani na utendakazi wake,” akaongeza Oruo.