Michezo

Ushindi wa Community Shield washawishi Aubameyang kusalia Arsenal

August 30th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Mikel Arteta amesema ushindi wa 5-4 uliosajiliwa na Arsenal dhidi ya Liverpool kupitia penalti kwenye Community Shield mnamo Jumamosi utamshawishi zaidi nahodha Pierre-Emerick Aubameyang, 31, kutia saini mkataba mpya ugani Emirates.

Mchango wa Aubameyang ambaye ana mwaka mmoja pekee kwenye mkataba wake wa sasa na Arsenal ulihisika pakubwa uwanjani Wembley, Uingereza.

Aliwaweka Arsenal uongozini kisha kufunga penalti ya ushindi katika mechi hiyo iliyokamilika kwa sare ya 1-1 mwishoni mwa dakika 90. Liverpool walisawazisha kupitia kwa kiungo mvamizi mzawa wa Japan, Takumi Minamino.

“Huu ni wakati bora zaidi wa kuwa mchezaji wa Arsenal,” akasema Aubameyang ambaye pia alifunga mabao mawili katika ushindi wa 2-1 waliousajili dhidi ya Chelsea katika fainali ya Kombe la FA ugani Wembley mnamo Agosti 1.

Nyota huyo mzawa wa Gabon amefungia Arsenal jumla ya mabao 70 kutokana na mechi 109 ambazo amezisakata tangu aagane na Borussia Dortmund ya Ujerumani kwa kima cha Sh7.2 bilioni mnamo Januari 2018.

Aubameyang alipokezwa utepe wa unahodha wa Arsenal mnamo Novemba 2019 baada ya utovu wa nidhamu kumfanya Granit Xhaka kupokonywa ukapteni na aliyekuwa kocha wa Arsenal, Unai Emery,

“Kazi yangu ni kujaribu kumsadikisha Aubameyang kwamba amejipata katika kikosi kizuri kwa wakati ufaao. Nadhani tayari ameamini hivyo na kinachosalia ni kurasimisha kandarasi mpya. Hilo ni jambo litakalohitaji muda zaidi,” akasema Arteta ambaye amechangia pakubwa ufufuo wa makali ya Arsenal.

“Walistahili kushinda. Kile ambacho Arteta amekifanyia kikosi cha Arsenal kinafurahisha. Kwa hakika, naona Arsenal wakiwa tishio kwa wapinzani wakuu wa Uingereza na bara Ulaya msimu ujao kwa sababu wanaimarika kwa kiwango cha kutisha,” akasema kocha Jurgen Klopp wa Liverpool.

Ingawa Liverpool walikosa huduma za beki Trent Alexander-Arnold na kiungo Jordan Henderson, Klopp aliwajibisha kikosi chenye wanasoka wa haiba waliokuwa na uwezo wa kupepeta Arsenal iliyokosa maarifa ya mafowadi mahiri Nicolas Pepe na Alexandre Lacazette.

Aubameyang kwa sasa ndiye mchezaji wa pili baada ya Alexis Sanchez wa Inter Milan kufungia Arsenal mabao matano ugani Wembley.

Sogora huyo ambaye pia amewahi kuchezea AC Milna na AS Monaco, alifunga pia mabao mawili katika ushindi wa 2-0 uliowezesha Arsenal kuwabandua Manchester City kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA ugani Wembley mnamo Julai.

Alipoulizwa kuhusu mustakabali wake ugani Emirates, Aubameyang alisema: “Tutaona jinsi mambo yatakavyokuwa. Tunaimarika na kikosi bado kinasukwa. Kuna kazi ya kufanywa na nina furaha sana.”

Arsenal kwa sasa wameibuka washindi wa Community Shield mara 16 na wamelitwaa taji hilo mara nne katika kipindi cha misimu saba iliyopita. Manchester United wanajivunia kutawazwa mabingwa mara 21, mara sita zaidi kuliko Liverpool.

Liverpool ndicho kikosi cha kwanza katika historia kupoteza taji la Community Shield mara mbili mfululizo kupitia mikwaju ya penalti. Hii ilikuwa pia mara ya kwanza kwa Liverpool tangu 1983 na 1984 kushiriki mechi ya Community Shield kwa misimu miwili mfululizo bila kuibuka washindi.

Arsenal wameibuka wafalme wa Community Shield mara saba wakishiriki kipute hicho baada ya kunyanyua ubingwa wa Kombe la FA.

Arsenal ndicho kikosi cha pili baada ya Man-United (mara tano) kutawazwa mabingwa wa Community Shield zaidi ya mara moja kupitia mikwaju ya penalti.