Uweza Queens inavyowapa vipusa fursa ya kunoa makali yao
Na PATRICK KILAVUKA
UWEZA Queens, timu ya soka ya wanadada inayotesa mtaani Kibra, Nairobi ilistawishwa mwaka 2017.
Ina kikosi cha wachezaji kumi na tisa ambao wananolewa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Toi na kupigia michuano ya ligi ya FKF, kinadada ya Kanda ya Nairobi (NWL) uwanja wa Woodley.
Iliazimia kuwapa vipusa fursa ya kusakata kabumbu katika mazingira yafaao na kubadilisha maisha yao kupitia kutumia vipaji vya masomo na talanta.
Malengo ya timu hii yanaonekana kutimia kwa sababu wasichana ambao wamebahati mithili ya mtende, hupata elimu ya shule ya msingi na ya upili kupitia mpango maalum wa ufadhili kupitia Uweza. Hata wengine hupata fursa ya kucheza soka ughaibuni.
Miongoni mwa wale ambao wameonja tayari matunda hayo ya kukuza talanta ni Matilda Muhonja ambaye amewahi kutalii Uholanzi baada ya kupata ufadhili akiwa kidato cha pili Shule ya Upili ya Kibuon, Kaunti ya Migori.
Wengine ambao wanafadhiliwa na Uweza baada ya huduma zao za kandanda kunaswa na kupigia chapuo taaluma yao ya soka ni Medina Abubakhari (miaka 12), Siama Mohammed, Joyce Wanuna (Shule ya upili ya Kibuon) miongoni mwa wengine.
Wanaisifia kuwa mkombozi wa maisha yao kwa kuwalipia karo. Fauka ya hayo, imewawezesha kujiepusha na marafiki wabaya, madawa na hata kuwa zizi mbadala la kuleta matumaini katika maisha yao.
Uweza inalenga wasichana wapevu masomoni kuendeleza ndoto ya kupata elimu wakikuza vipawa vyao vya kabumbu. Japo kwa kuthamani pia vipaji adimu, wale ambao wameruzukiwa hawajasazwi wanaporidhisha Uweza kwamba, vipawa vyao vya soka vina makali lakini wanakosa kupata fursa kuvichochea au kuviangazia.
Malengo mingine ambayo yanakumbatiwa ni kuwanidhamisha, kuwakuza kimaadili, kuwatahadharisha na mimba za mapema na kadhalika.
Chini ya benchi ya kocha Dennis Odhiambo (mchezaji wa zamani wa timu ya madume ya Uweza) na timu meneja Charles Khaindi imepimwa uwezo wake kupitia kusajiliwa katika ligi iliyotajwa awali.
Kufika kuandika kwa makala, ilikuwa imejitosa ugani mara tano. Iliichabanga Kibagare Girls 2-1 kabla kuilipua Archivers Ladies 2-1 uwanjani Kihumbuini.
Hata hivyo, ilipigwa katika mechi yake dhidi ya Kangemi Ladies 1-0, kukomolewa na Beijing Raiders 2-0 ugani Mathare Depot kisha kusazwa na Amani Queens 2-0 katika mechi ambayo ilipepetewa uwanja wa Nakeel.
Wachezaji ambao walisajiliwa kupiga jeki kikosi in kipa Joy Adhiambo, madifenda Warda Mayungi na Anne Aanyango na mastraika Cindy Aluoch na Susan Kwamboka
Mipango ya timu sasa ni kujiimarisha zaidi kupanda ngazi ya ligi ya daraja ya juu na kuendelea kulea talanta za wanasoka hawa ambao wamechongwa tangu wengine wakiwa na miaka ya chini ya miaka kumi na miwili.