Van Dijk amtetea Salah, asema ataamka kwa kishindo
NA CECIL ODONGO
MLINZI wa Liverpool Virgil Van Dijk amejitokeza na kumtetea mshambulizi Mohamed Salah ambaye miguu yake msimu huu wa 2018/19 imeingia kutu na hafungi mabao jinsi ilivyokuwa msimu jana wa 2017/18.
Salah, raia wa Misri amekuwa na wakati mgumu baada ya kukosa kuona lango la wapinzani kwenye mechi saba mfululizo, hali ambayo imepelekea wapinzani wao Manchester City kuwaandama kwa karibu huku msimu huu wa Ligi ya Uingereza(EPL) ukielekea kufika tamati.
Hata hivyo Van Dijk amesema ana wingu la matumaini kuwa Sala atarejelea ubora wake wa msimu uliopita na kuwadhihirishia wakosoaji wake vinginevyo.
“Watu wanaweza kusema hekaya yote na wanachotaka ila nawahakikishia Salah atarejelea fomu yake na kutusaidia kutwaa ubingwa wa EPL. Yeye ni mchezaji ambaye kila timu inawania kuwa naye kama mpira wa kona,”
“Mabao yatakuja na sisi humweleza waziwazi kuwa kama mshambulizi, hafai kutetereka wala kuwa na wasiwasi kwasababu kuna kipindi fomu ya mchezaji lazima ishuke,” Virgil akaeleza mtandao wa Liverpool.
Msimu wa 2018, Salah aliweka rekodi kwa kuifungia Liverpool jumla ya mabao 44 kwenye ligi, Klabu Bingwa Barani Uropa(UEFA) na Kombe la Shirikisho la Uingereza(FA). Alifunga mabao muhimu kwenye kipute cha UEFA kilichosaidia Liverpoo kufika fainali kwa mara ya kwanza tangu 2004 ingawa walipoteza kwa walioibuka mabingwa, Real Madrid.
Msimu huu, Salah amefunga mabao 17 kwenye EPL na 44 katika mashindano yote Liverpool imewajibikia.