Van Dijk pazuri kumpokonya Salah tuzo ya mwanasoka bora EPL
Na GEOFFREY ANENE
BEKI Virgil van Dijk anapigiwa upatu kushinda tuzo ya Mwanasoka Bora nchini Uingereza (PFA) msimu 2018-2019 anapoendelea kuonyesha ubabe wake katika safu ya ulinzi ya klabu ya Liverpool.
Taji hili linashikiliwa na mchezaji mwenza na mvamizi matata Mohamed Salah, ambaye siku chache zilizopita alihifadhi ubingwa wa Mwanasoka Bora wa Bara Afrika jijini Dakar, Senegal.
Wachezaji wengine wa Liverpool ambao wamewahi kunyakua taji la Mwanasoka Bora wa msimu nchini Uingereza tangu lianzishwe msimu 1973/1974 ni Luis Suarez (2013/2014), Steven Gerrard (2005/2006), John Barnes (1987/1988), Ian Rush (1983/1984), Kenny Dalglish (1982/1981) na Terry McDermott (1979/1980).
Mholanzi Dijk alikuwa na asilimia kubwa ya kutwaa taji hilo mwanzoni mwa msimu, ingawa umaarufu umepungua msimu ukiendelea.
Liverpool inasalia klabu iliyofungwa mabao machache zaidi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (10). Chelsea, ambayo inaikaribia imefungwa mabao 16. Kufikia wakati huu msimu 2017-2018, Liverpool ilikuwa imekubali nyavu zake kuchanwa mara 25.
Tovuti ya Livepool Echo inasema wanaomkaribia Dijk katika vita vya kuibuka Mwanasoka Bora wa msimu nchini Uingereza ni David Silva (Manchester City) akifuatiwa na Eden Hazard (Chelsea), Harry Kane (Tottenham Hotsopur), Salah (Liverpool) na Raheem Sterling (Manchester City) katika usanjari huo.
Msemaji wa kampuni moja ya kubashiri mshindi wa tuzo hii amenukuliwa na tovuti hiyo akisema kwamba Dijk amechangia pakubwa katika kulinda ngome ya Liverpool.
Msemaji George Elek kutoka kutoka Oddschecker anasema, “Ukubwa wa mchango wa Virgil van Dijk umeonekana sana msimu huu. Amebadilisha kabisa safu ya ulinzi ambayo msimu uliopita ilikuwa inavuja kabla awasili…Atakuwa mshindi mstahiki, bila yeye ni vigumu kusema Liverpool ingekuwa bado katika vita vya kuwania taji.”