Vikosi vya Italia vyaafikiana kukamilisha ligi ya Serie A msimu huu
Na CHRIS ADUNGO
KLABU zote 20 za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) zimeafikiana kukamilisha msimu huu wa 2019-20 kwa kushiriki michuano yote iliyosalia katika kivumbi hicho kabla ya shughuli zote za michezo kusitishwa mwanzoni mwa Machi kutokana na virusi vya corona.
Haya yaliiafikiwa katika mkutano wa jana uliochochewa na ripoti zilizodai kwamba Torino na Brescia walikuwa radhi kugomea kampeni za msimu huu iwapo kipute cha Serie A kingerejelewa kabla ya corona kudhibitiwa vilivyo.
Hata hivyo, imefichuka kwamba kwa sasa kila kikosi ligini humo kinapania kushuhudia msimu huu ukirejelewa wakati wowote kuanzia Mei 18 na kutamatika rasmi.
Hata hivyo, Waziri Mkuu wa Italia, Vincenzo Spadafora ameonya kwamba hakuna uhakika ambao umetolewa na Serikali hadi kufikia sasa kuhusu uwezekano wa kukamilishwa kwa kampeni za Serie A muhula huu.
Baada ya Serikali ya Ufaransa kufutilia mbali msimu mzima wa Ligue 1 na kusitisha zaidi shughuli zote za michezo nchini humo hadi Septemba 2020, gazeti la ‘The Sun’ limedokeza kwamba Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa anasukuma viongozi wenzake katika nchi tofauti za bara Ulaya kufuata mkondo wake.
Hata hivyo, Kinara wa Shirikisho la Soka la Italia, Gabriele Gravina ameapa kutolegeza kamba katika juhudi za kushawishi Serikali kushirikiana na washikadau wote kufanikisha kampeni za Serie A muhula huu.
Italia ndilo taifa la bara Ulaya lililoathiriwa zaidi na virusi vya corona baada ya kuripotiwa kwa zaidi ya vifo 28,000 na maambukizi zaidi ya 205,000.
Isitoshe, nyota wa Juventus, Paulo Dybala amepatikana sasa akiwa na virusi vya corona mara nne baada ya kufanyiwa vipimo katika vipindi mbalimbali chini ya majuma sita yaliyopita.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi na Shirikisho la Soka la Italia (FIGC), kivumbi cha Serie A kimepangiwa kuanza upya wakati wowote kati ya Mei 27 na Juni 2, huku kikitakiwa kutamatika rasmi kufikia mwanzo wa wiki ya kwanza ya Agosti 2020.
Wachezaji wote wametakiwa kuripoti kambini kufikia Mei 4. Mechi 12 zilizosalia katika Serie A muhula huu zitasakatwa ndani ya viwanja vitupu.
Kivumbi cha Serie A kiliahirishwa mnamo Machi 9 na wachezaji kadhaa wa ligi hiyo wakapatikana na virusi vya homa kali ya corona.
Miongoni mwao ni Daniele Rugani, German Pezzella, Patrick Cutrone, Dusan Vlahovic, Manolo Gabbiadini, Omar Colley, Albin Ekdal, Antonio La Gumina, Morten Thorsby, Fabio Depaoli, Dybala na Blaise Matuidi.