Michezo

Vinara wa CAF kukagua uwanja wa Nyayo baada ya ukarabati kukamilika

June 26th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na CHRIS ADUNGO

VINARA wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) wanatarajiwa kutua jijini Nairobi mnamo Julai au Agosti 2020 kwa lengo la kukagua uwanja wa Nyayo na kutathmini iwapo unafikia viwango vya kimataifa baada ya kufanyiwa ukarabati.

Ukaguzi wa awali wa CAF ulitarajiwa kufanyika Machi 2020, ila mpango huo ukavurugwa na mlipuko wa virusi vya ugonjwa wa Covid-19.

Kamati Andalizi ya Mechi za Kimataifa za CAF (IMOC) imezuru uwanja wa Nyayo na kutathmini hatua ambazo zimepigwa katika juhudi za kuukarabati uwanja huo. Kamati hiyo ililenga pia kubaini iwapo shughuli zinazoendelea ugani humo zinawiana na mwongozo uliotolewa na CAF na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

“Tumekagua vyumba vya wachezaji kubadilishia sare, vyumba vya matibabu ya dharura, vyumba vya upeperushaji wa matangazo na hali ya usalama uwanjani wakati wa mashindano. Sasa tutaanza kuandaa ripoti yetu kabla ya ujio wa vinara wa CAF mnamo Julai, Agosti au pindi masharti ya usafiri wa kimataifa yatakapolegezwa,” akasema Mwenyekiti wa IMOC, Michael Ouma.

Mnamo Mei 2020, Waziri wa Michezo Amina Mohamed alithibitisha kuwa shughuli za ukarabati katika uwanja wa Nyayo zilikuwa zinaelekea kukamilika baada ya kipindi cha takriban miaka mitatu.

Alisema uwanja huo ulikuwa tayari kufunguliwa kwa mapambano mbalimbali zikiwemo mechi za Ligi Kuu ya KPL na soka ya kimataifa wakati wowote kuanzia Julai, na unapigiwa upatu kuwa mwenyeji wa makala ya kwanza ya Riadha za Dunia za Continental Tour zilizoahirishwa hadi Septemba 26, 2020 kutokana na janga la virusi vya corona.

Kati ya mabadiliko ambayo kwa sasa yanachora sura mpya ya uwanja wa Nyayo ambao ni wa pili kwa ukubwa baada ya MISC Kasarani, ni mpangilio mpya wa viti vilivyopakwa rangi za bendera ya Kenya.

“Baadhi ya sehemu zipo katika hatua za mwisho za ukarabati na takriban asimilia 99 ya kazi ishafanyika. Shughuli zilizosalia huenda zikakamilika chini ya kipindi cha wiki mbili zijazo na uwanja kukabidhiwa kwa Sports Kenya mwishoni mwa Juni 2020,” alisema Amina.

Uwanja wa Nyayo ulio na uwezo wa kubeba takriban mashabiki 30,000 walioketi ulifungwa mnamo 2017 kwa ukarabati uliokusudiwa kuuweka tayari kwa minajili ya fainali za CHAN 2018.

Japo kivumbi hicho kilitarajiwa kufanyika humu nchini, mwendo wa kobe katika ukarabati wa viwanja ulichangia Kenya kupokonywa haki za kuwa mwenyeji wa kipute hicho kilichohamishiwa baadaye nchini Morocco mnamo Januari 12 – Februari 4, 2018.

Baadhi ya sehemu zinazosalia kushughulikiwa uwanjani humo ni kuwekwa kwa taa mpya na zulia jipya la kisasa katika eneo la wanariadha kukimbilia.

Mbali na vyumba viwili vya marefa, miongoni mwa vyumba vipya ambavyo pia vimejengwa kwa sasa katika uwanja wa Nyayo ni viwili vitakavyotumiwa kuwafanyia wanariadha vipimo vya kubaini iwapo wametumia dawa za kusisimua misuli na vinne vya wanamichezo kubadilishia sare.