Michezo

Vipusa wa Uingereza roho juu wakivizia USA

July 2nd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

LYON, UFARANSA

KOCHA Phil Neville wa timu ya taifa ya soka ya wanawake nchini Uingereza amesema kwamba kikosi chake kitakuwa kimefeli iwapo kitashindwa kuwapepeta Amerika kwenye nusu-fainali na kutwaa Kombe la Dunia hatimaye.

Uingereza almaarufu ‘The Lionesses’, wanashuka dimbani leo Jumanne kuvaana na mabingwa watetezi USA katika gozi kali la nusu-fainali litakalowakutanisha jijini Lyon, Ufaransa.

Jumatano itakuwa zamu ya Uholanzi kupimana ubabe na Uswidi katika nusu-fainali nyingine.

Uingereza ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu duniani hawajawahi kufanikiwa kupita hatua ya nne-bora kwenye makala manne yaliyopita ya fainali za kuwania ubingwa wa Kombe la Dunia.

“Haijalishi ni nani atashindwa katika nusu-fainali ya leo. Ninavyojua ni kwamba kikosi changu kimejiandaa vya kutosha na wachezaji wa Uingereza hawana sababu ya kutoyazima makali ya USA,” akatanguliza Neville.

“Haijalishi ni nani ataambulia nishani ya fedha au shaba. Nijuavyo ni kwamba vipusa wangu watakuwa wamefeli sana iwapo watashindwa kuwazamisha USA na kutwaa umalkia wa Kombe la Dunia mwaka huu,” akasema nyota huyo wa zamani wa Manchester United.

Mara ya mwisho kwa Uingereza kutinga nusu-fainali za mapambano ya haiba kubwa ni 2017 katika kivumbi cha Euro kilichowashuhudia wakipokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Uholanzi waliokuwa wenyeji wa fainali hizo.

“Wachezaji wangu kwa sasa wanatawaliwa na kiu ya kutia taji kikapuni. Iwapo hatutasajili matokeo ya kuridhisha dhidi ya USA leo Jumanne, basi tutakuwa tumewaangusha mashabiki wetu ambao kubwa zaidi katika matarajio yao ni kurejea nyumbani tukiwa na kombe mikononi,” akasema.

Japan yaipiga Uingereza

Mnamo 2015, Uingereza walipepetwa na Japan katika nusu-fainali za Kombe la Dunia.

Hata hivyo, waliwazidi Ujerumani maarifa katika mchuano wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu na nne.

Hadi kufikia sasa, huo ndio ufanisi mkubwa zaidi kuwahi kuvunwa na kikosi hicho katika historia ya fainali za Kombe la Dunia.

Kwa upande wao, USA ambao ni mabingwa mara tatu wa Kombe la Dunia wanajivunia rekodi bora zaidi dhidi ya Uingereza. Miamba hao wa soka wamepoteza mechi moja pekee kati ya tano zilizopita dhidi ya Uingereza.