Michezo

Wakenya waingia tenisi ya Afrika kwa dhahabu 3 na fedha za kanda

Na GEOFFREY ANENE January 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WENYEJI Kenya wanatupia jicho mashindano ya Afrika baada ya kunyakua dhahabu ya timu katika vitengo vya wasichana na wavulana wasiozidi umri wa miaka 16 pamoja na wasichana wasiozidi miaka 14, kwenye mashindano ya tenisi ya Afrika Mashariki (Zoni ya Nne) katika uga wa Nairobi Club jijini Nairobi.

Kenya pia aliridhika na nishani ya fedha ya wavulana wasiozidi umri wa miaka 14 kwenye mashindano hayo ya karibu wiki mbili yaliyoanza Januari 12, 2025 na kutamatika Alhamisi.

Jeff Okuku/Ayush Bhandari walishindia Kenya dhahabu ya U-16 (wavulana). Walitawala mechi ya wachezaji wawili kila upande ya kuamua mshindi kwa kupepeta Francis Bireha/Miki Igiraneza kutoka Burundi kwa seti mbili bila jibu za 6-2, 6-4.

Okuku alitangulia kunyakua mechi ya kwanza ya mchezaji mmoja kila upande kwa kuchapa Bireha 6-1, 6-0 kabla ya Bhandari kuteleza 6-2, 4-6, 6-1 katika mchuano wa pili dhidi ya Igiraneza na kulazimisha ile ya wachezaji wawili kila upande kuchezwa ili kuamua mshindi.

“Nafurahi sana kuwa tumepokonya Burundi taji. Mwaka jana, walitupiga katika fainali mjini Bujumbura kwa hivyo ni furaha kubwa kuwa tumelipiza kisasi mbele ya mashabiki wetu,” akasema Okuku.

Bhandari alieleza kuwa kilichowasaidia kutwaa dhahabu hiyo ni kutibua makombora ya wapinzani na pia savu kuwakubali. “Mechi ya kuamua mshindi ilikuwa kali, lakini tulifaulu kuibuka na ushindi kutokana na kujituma vilivyo,” akaongeza.

Ilikuwa raha ilioje kwa kocha Rosemary Owino akisema mechi ilikuwa moto kutokana na Burundi kuleta mchezo wao bora katika fainali.

Katika fainali ya U-16 (wasichana), Kenya ilimaliza kazi katika mechi za mchezaji mmoja kila upande kupitia kwa Nancy Kawira na Seline Ahoya.

Seline Ahoya apiga mpira kwenye fainali yake uwanjani Nairobi Club mnamo Alhamisi. PICHA | HISANI

Ahoya aliweka Kenya kifua mbele 1-0 alipomwaga Yusra Irakoze (Burundi) 6-0, 6-1 katika mchuano wa kwanza. Kawira alikamilisha kazi kwa kukomoa Bebita Ishimwe (Burundi) 6-4, 6-4.

“Nilicheza vizuri sana na ninafurahia kuwa nilipatia Kenya uongozi kwa kushinda mechi ya kwanza. Niliongoza Kenya kutawala kitengo hiki mwaka jana na ninafurahia tena kufanya hivyo,” akasema Ahoya.

Kawira, ambaye alipiga Ahoya katika wiki ya kwanza ya mashindano hayo wakati wa mashindano ya wachezaji binafsi, alitosheka na alivyochangia katika Kenya kushinda mashindano ya timu hapo Alhamisi. “Nashukuru mashabiki kwa kujitokeza kwa wingi kutupatia motisha,” akaongeza Kawira.

Katika fainali ya U-14 (wasichana), Bathsheba Ogamba na mkazi wa Afrika Kusini Felicia Ouko walizidia Chantal Niyimbabazi na Marie Celia Kezakimana kutoka Burundi kwa seti mbili kavu. Ogamba alilemea Niyimbabazi 6-1, 6-2 naye Ouko akachapa Kezakimana 6-4, 6-2.

“Nimeridhika na jinsi nilicheza leo kwa sababu ilituwezesha kuibuka na ushindi baada ya mwenzangu kutawala mechi ya kwanza,” akasema Ouko anayepanga kurejea Afrika Kusini hapo Ijumaa.

Katika fainali ya U-14 (wavulana), Kenya ilijikakamua kadri ya uwezo wake na kuridhika na medali ya fedha baada ya Ayaan Quadros na Vihaan Bulsara kusalimu amri ya Waganda Cosmas Munguriek na Samuel Okello, mtawalia.

Kocha Edward Odokcen alifurahishwa na vijana wake kutoka Uganda walivyocheza. “Ni muda mrefu sijaona fainali moto na ya kusisimua kama hii. Ni mechi ambayo ingeenda upande wowote, lakini tulikuwa juu kidogo kiakili,” akasema Odokcen.

Naibu rais wa Shirikisho la Tenisi la Afrika (CAT) Wanjiru Mbugua, ambaye ni rais wa Shirikisho la Tenisi la Afrika Mashariki na Katibu wa Shirikisho la Tenisi Kenya, alieleza kufurahishwa na viwango vya ushindani vilivyoonyeshwa na washiriki.

“Mashindano haya yalikuwa ya kuingia ya Afrika ambayo pia Kenya itaandaa ya U-14 mwezi ujao. Nimefurahishwa na idadi ya timu zilizojitokeza kushiriki. Naweza kusema timu zote zilijitokeza. Zoni hii ina mataifa 12. Mataifa 10 yalijitokeza isipokuwa mawili ambayo hayakufanya hivyo kwa sababu ukosefu wa usalama katika mataifa hayo,” akasema Wanjiru.

Mataifa yaliyoshiriki ni Kenya, Burundi, Djibouti, Ethiopia, Eritrea, Rwanda, Somalia, Tanzania, Uganda na Ushelisheli. Mashindano ya Afrika U-14 ya uwanja wa udongo (AJCCC) ni Februari 24 hadi Machi 1 ugani Nairobi Club. Sudan na Sudan Kusini pia ziko Zoni ya Nne.