Wanasoka 7 walioishia kuwa masupastaa baada ya kutemwa na Chelsea
Na CHRIS ADUNGO
KILA mara Kevin De Bruyne au Mohamed Salah anapotawazwa Mchezaji Bora wa Mechi kutokana na matokeo yao ya kuridhisha, mashabiki wa Chelsea huingiwa na fadhaa, masikitiko na huzuni.
Kabla ya masupastaa hao kwa sasa kufikia walipo kwenye ulingo wa soka, waliwahi kuvalia jezi za Chelsea waliowaachilia wajitafutie hifadhi mpya kwingineko baada ya kutoridhisha vinara wa kikosi hicho uwanjani Stamford Bridge.
Hapa tunawaangazia wanasoka saba waliowahi kupuuzwa na Chelsea kisha wakayomemea kwingineko na kuwa masogora wa kutegemewa.
KEVIN DE BRUYNE
Mbelgiji huyu kwa sasa ni miongoni mwa viungo bora zaidi duniani. Kwa ubora anaojivunia kwa sasa, haiaminiki kwamba De Bruyne aliwahi kushindwa kabisa kutamba kambini mwa Chelsea.
Baada ya kusajiliwa na mnamo 2011-12 kutoka Genk ya Ubelgiji, nyota huyo wa sasa wa Manchester City aliwajibishwa na Chelsea mara mbili pekee kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Baada ya kujipata katika ulazima wa kusugua benchi, alitumwa hadi Werder Bremen ya Ujerumani kwa mkopo kabla ya kupigwa mnada hadi Wolfsburg waliomtwaa kwa Sh2.3 bilioni pekee.
Akiwa huko, nyota ya De Bruyne iling’aa zaidi na akasajiliwa na Man-City kwa kima cha Sh7.7 bilioni mnamo 2015.
Sogora huyo stadi wa kusuka pasi anajivunia kutia kapuni mataji mawili ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) akichezea Man-City.
MOHAMED SALAH
Alijiunga na Chelsea kutoka FC Basel ya Uswisi mnamo 2014 na akachezeshwa mara 13 katika mechi zilizomshuhudia akifunga mabao mawili pekee ligini.
Mnamo 2015 na 2016, fowadi huyo raia wa Misri alitumwa kwa mkopo hadi Fiorentina na AS Roma kabla ya kujiunga na Roma kwa mkataba wa kudumu uliogharimu Sh1.5 bilioni pekee.
Baada ya msimu mmoja pekee nchini Italia, Liverpool walimrejesha Salah kwenye soka ya EPL baada ya kumsajili kwa kima cha Sh5.1 bilioni.
Katika msimu wake wa kwanza uwanjani Anfield, Salah alivunja rekodi ya ufungaji katika EPL kwa kupachika wavuni idadi kubwa zaidi ya mabao katika ligi hiyo ya mechi 38 kwa msimu.
Katika msimu wake wa pili, Salah aliongoza Liverpool kukamilisha kampeni za EPL katika nafasi ya pili na kutwaa ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).
Ni hadi 2019-20 akiwa katika msimu wake wa tatu ugani Anfield ambapo Salah, ambaye kwa sasa ni miongoni mwa wavamizi bora zaidi duniani, alisaidia Liverpool kutawazwa mabingwa wa taji la EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.
ARJEN ROBBEN
Alipoingia katika sajili rasmi ya Chelsea mnamo 2004, baadhi ya mashabiki wa Chelsea walihisi kwamba walikuwa wamejinasia huduma za fowadi matata zaidi hata kuliko Cristiano Ronaldo katika ulingo wa soka enzi hizo.
Mambo yalionekana hivyo kwa kipindi kifupi cha msimu wa kwanza wa Mholanzi huyo ugani Stamford Bridge. Alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwezi mwanzoni mwa msimu wake kambini mwa Chelsea na akasaidia kikosi hicho kutwaa taji la EPL kwa mara ya kwanza baada ya miaka 50.
Baada ya miwili pekee, uhusiano kati ya Robben na kocha Jose Mourinho ulivurugika na sogora huyo akabanduka Chelsea na kutua Real Madrid. Japo nyota yake haikung’aa sana ugani Santiago Bernabeu, alianza kutamba zaidi alipotua nchini Ujerumani kuvalia jezi za Bayern Munich.
Robben aliingia katika orodha ya wanasoka bora zaidi wa muda wote katika Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) na akasaidia waajiri wake kutwaa mataji manane ya Bundesliga katika kipindi cha misimu 10, likiwemo taji la UEFA mnamo 2013.
ROMELU LUKAKU
Baada ya kujiunga na Chelsea akitokea Anderlecht ya Ubelgiji mnamo 2011, Lukaku alitazamiwa kuwa miongoni mwa wanasoka mahiri zaidi duniani.
Hata hivyo, aliwajibishwa na Chelsea katika mechi 10 pekee za EPL kabla ya kutumwa West Bromwich Albion kwa mkopo kisha huduma zake kutwaliwa rasmi na Everton.
Lukaku alidhihirisha ukubwa wa uwezo wake kwa kupachika wavuni jumla ya mabao 53 kutokana na mechi 110 alizochezea Everton. Kuimarika huko kuliwashawishi Manchester United kumsajili kwa kima cha Sh10.5 bilioni.
Ingawa hakuridhisha sana uwanjani Old Trafford, aliyoyomea Italia kuvalia jezi za Inter Milan ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte. Akiwa Inter, Lukaku alifufua makali yake na akafunga jumla ya mabao 41 kutokana na mechi 58 za Ligi Kuu ya Italia (Serie A).
NATHAN AKE
Beki huyo raia wa Uholanzi alijiunga na kikosi cha chipukizi wa Chelsea kutoka Feyenoord mnamo 2011 kabla ya kukwezwa ngazi hadi timu ya wazima mwaka mmoja baadaye.
Hata hivyo, aliwajibishwa katika mechi saba pekee uwanjani Stamford Bridge kabla ya kutumwa kwa mkopo hadi Reading, Watford na Bournemouth waliompa mkataba wa kudumu.
Ingawa yalikuwa matamanio ya Bournemouth kujivunia huduma zake zaidi baada ya miaka mitatu ya kwanza iliyomshuhudia akiwajibishwa katika zaidi ya mechi 100 za EPL, Ake alijiunga na Man-City kwa kima cha Sh5.6 bilioni mwishoni mwa msimu wa 2019-20.
Akiwa Man-City kwa sasa, Ake ni miongoni mwa wachezaji wanaotegemewa pakubwa na kocha Pep Guardiola uwanjani Etihad.
NEMANJA MATIC
Baada ya kusajiliwa kutoka Kosice ya Slovakia mnamo 2009, Matic alitarajiwa kuwa nyota tegemeo kambini mwa Chelsea.
Hata hivyo, kiungo huyo raia wa Serbia aliwajibishwa mara mbili pekee katika EPL kabla ya kutumwa kwa mkopo hadi kambini mwa Vitesse nchini Uholanzi.
Baada ya kuhudumu ugani Stamford Bridge kwa miaka miwili, alijiunga na Benfica mnamo 2011 na kuondoka kwake kukachochea Chelsea kusajili David Luiz.
Nyota ya Matic ilipoanza kung’aa zaidi kambini mwa Benfica, Chelsea walimsajili upya mnamo 2014 kwa Sh2.9 bilioni. Fedha hizo zilikuwa mara 20 zaidi ya zile ambazo Chelsea waliweka mezani kwa minajili ya huduma za Matic walipomsajili mara ya kwanza. Matic alijiunga baadaye na Manchester United ambao wamekuwa wakimtegemea katika safu ya kati tangu 2017.
TIAGO MENDES
Nyota huyu mzawa wa Ureno aliondoka Chelsea baada ya msimu mmoja pekee kabla ya kuyoyomea Uhispania kuvalia jezi za Atletico Madrid waliomfanya kuwa miongoni mwa viungo bora zaidi duniani.
Kabla ya kutumwa kwa mkopo kisha kusajili rasmi na Atletico, ushirikiano kati ya Tiago na Gabi uliimarisha zaidi safu ya kati ya kikosi cha kocha Diego Simeone na kufanya Atletico miongoni mwa vikosi vya kuogopewa zaidi katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).
Tiago alikuwa sehemu ya kikosi cha Atletico kilichokomesha ukiritimba wa Barcelona na Real Madrid kwenye La Liga mnamo 2014. Ilikuwa mara ya kwanza kwa Atletico kutia kapuni ubingwa wa taji hilo baada ya miaka 18 na wakatinga pia fainali ya UEFA.
Tiago aliwajibishwa na Atletico mara 250 na akasaidia kikosi hicho kutwaa ubingwa wa La Liga, Europa League na Copa del Rey kisha kutinga fainali mbili za UEFA.