Wanyama aeleza kiini cha uhamisho kutoka Spurs kufeli
Na MWANDISHI WETU
HUKU sehemu ndogo ya mashabiki sasa ikitaka Victor Wanyama apokonywe unahodha wa timu ya taifa ya Kenya, kiungo huyu wa Tottenham Hotspur kwa mara ya kwanza amefunguka na kuzungumzia uhamisho wake hadi Club Brugge uliofeli kutimia.
Wanyama, ambaye alifikisha umri wa miaka 28 wakati wa Kombe la Afrika nchini Misri mwezi Juni, ameshuka sana katika orodha ya wachezaji wanaotumiwa na Spurs katika safu ya kati.
Hali hiyo imechangiwa na kusumbuliwa na majeraha ya magoti.
Kocha Mauricio Pochetino hata aliamua kuwanunua Tanguy Ndombele na Giovani Lo Celso wakati wa kipindi kirefu cha uhamisho nchini Uingereza mwezi Agosti akinuia kumwondoa Wanyama katika kikosi chake.
Idara hiyo ya katikati pia ina wachezaji Harry Winks, Moussa Sissoko na Eric Dier pamoja na Dele Alli na Christian Eriksen. Kutokana na wingi wa viungo hawa, Wanyama hata amejipata akisukumwa chini ya orodha hiyo na chipukizi Oliver Skipp, ambaye amekuwa akijumuishwa katika vikosi vya siku ya mechi badala ya Mkenya huyu.
Vyombo vya habari nchini Uingereza vinasema kuwa Wanyama alikaribia sana kuhamia klabu ya Ubelgiji ya Club Brugge kabla ya kipindi cha uhamisho kufungwa Septemba 2 barani Ulaya. Club Brugge inaongozwa na Philippe Clement, ambaye alicheza na Wanyama katika klabu ya Beerschot miaka 10 iliyopita.
Hata hivyo, uhamisho wa Wanyama hadi Club Brugge haukufaulu kwa hivyo nahodha huyo wa Kenya akasalia jijini London na klabu yake ya Spurs.
“Mambo yalikuwa yanaenda sawa, lakini kwa bahati mbaya uhamisho haukukamilika. Hata hivyo, lazima nisahau hilo na nijikakamue vilivyo mazoezini kutafuta makali yangu nikisubiri fursa ya kuchezea timu yangu ya Spurs,” alinukuliwa akisema Oktoba 13.
Uchezaji
Wanyama amekuwa uwanjani dakika 23 pekee kuchezea Spurs ligini msimu huu. Spurs imesakata mechi nane za ligi. Inashikilia nafasi ya tisa kwa alama 11. Itaalika Watford inayovuta mkia kwenye ligi hiyo ya klabu 20 bila ushindi katika mechi yake ijayo mnamo Septemba 19.
Wanyama, ambaye kakaye McDonald Mariga yuko uwanjani kuwania ubunge wa Kibra jijini Nairobi mnamo Novemba 7, alichezea Spurs dakika 90 katika soka ya League Cup dhidi ya Colchester United.
Hata hivyo, Spurs ilibanduliwa kutoka dimba hilo ilipopoteza dhidi ya Colchester kwa njia ya penalti 4-3 mnamo Septemba 24.