Michezo

Wanyama asherehekea kutimiza umri wa miaka 28 hatima yake Spurs ikisalia gizani

June 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MWANDISHI WETU

KIUNGO Victor Wanyama alisherehekea Jumanne kufikisha umri wa miaka 28, huku ripoti zikidai hayuko tayari kuhama Tottenham Hotspur inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Alipokea jumbe nyingi za kumtakia kheri njema pamoja na maisha marefu na pia kutembelewa na kaka yake ambaye ni McDonald Mariga.

Hata hivyo, uvumi umekuwa ukienea kwamba nyota huyu wa Kenya atauzwa katika kipindi hiki kirefu cha uhamisho.

Inasemekana kwamba nahodha huyu wa Harambee Stars anapanga kuendelea kuchezea Spurs, ambayo ilimaliza Klabu Bingwa Ulaya katika nafasi ya pili nyuma ya Liverpool na EPL katika ya nne nyuma ya Manchester City, Liverpool na Chelsea zilizokamilisha ligi katika nafasi tatu za kwanza msimu 2018-2019.

Wanyama amekuwa akisumbuliwa na majeraha ya goti ambayo yaliyomfanya achezee Spurs mechi 13 pekee ligini msimu 2018-2019 kati ya 38 zinazochezwa na kila klabu katika ligi hiyo ya timu 20.

Mchezaji huyu wa zamani wa klabu za Nairobi City Stars, AFC Leopards (Kenya), Helsingborg (Uswidi), Beerschot (Ubelgiji), Celtic (Scotland) na Southampton (Uingereza) anakabiliwa na hatari ya kuuzwa ama kutumiwa kwa uchache zaidi Spurs ikifaulu kununua Mfaransa Tanguy Ndombele (Lyon, Ufaransa) na raia wa Argentina Giovani Lo Celso (Real Betis, Uhispania), ambao inamezea mate. Wanyama alijiunga na Spurs mwaka 2016 kwa Sh1.4 bilioni kutoka Southampton akimfuata kocha wake wa zamani Mauricio Pochettino.