Michezo

Warembo wa Kenya wala sare dhidi ya Ghana

August 13th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imepata alama moja muhimu dhidi ya Ghana japo kwa jasho katika mechi yake ya pili ya kina dada kwenye mchujo wa mpira wa magongo wa Afrika wa kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2020 ambayo imetamatika 1-1 nchini Afrika Kusini, Jumanne.

Rhoda Kuira (pichani) alifungia Kenya bao la mapema katika dakika ya saba kutokana na kona fupi.

Hata hivyo, kutoka hapo warembo wa kocha Tom Olal walishambuliwa hadi kipenga cha mwisho.

Mashambulizi makali ya Ghana yalishuhudia ikisawazisha 1-1 kupitia kwa Mavis Berko kutokana na kona fupi.

Kenya ilipata kona tatu dhidi ya nane za Ghana, ambayo mara tatu ilinyimwa bao na kipa aliyekuwa macho michumani. Wakenya waliponea mara kadhaa kuadhibiwa na Ghana kwa kupoteza mipira kwa urahisi.

Ghana ilitumia kasi ya juu na ilionana zaidi kuliko Kenya, lakini mbali na kipa wa Kenya kufanya kazi ya ziada langoni kuondosha hatari ikiwemo katika dakika ya 43, 51 na 52, Ghana ilikosa bahati.

Matokeo haya yaliendeleza rekodi nzuri ya Kenya kutoshindwa na Ghana katika mechi za kufuzu kushiriki Olimpiki hadi mechi nne.

Ilitoka 3-3 na Ghana katika mechi ya mchujo wa kuingia Olimpiki mwaka 2016 ilipomaliza katika nafasi ya tatu nchini Afrika Kusini mwaka 2015.

Pia, ilitoka 1-1 na Ghana katika mechi ya makundi ya michuano ya mwaka 2011 nchini Zimbabwe ambayo ilikuwa ya kufuzu kushiriki Olimpiki mwaka 2012.

Mara ya kwanza

Mara ya kwanza mataifa haya yalikutana katika mechi ya kufuzu kushiriki Olimpiki ilikuwa mwaka 2007 wakati Kenya ilichapa Ghana 1-0 jijini Nairobi katika mechi za makundi.

Hapo Jumanne, Kenya na Ghana ziliingia uwanjani na motisha ya kufungua kampeni zao kwa ushindi mnamo Agosti 12.

Kenya, ambayo inatafuta tiketi ya kushiriki mpira wa magongo wa wanawake kwa mara ya kwanza katika Olimpiki, ililima Namibia 1-0 kupitia bao la Grace Makokha nayo Ghana ikazaba Zimbabwe 3-1.

Kenya itamenyana na Zimbabwe katika mechi yake ijayo mnamo Agosti 15 kabla ya kukamilisha kampeni yake dhidi ya miamba Afrika Kusini mnamo Agosti 17