• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Warembo wa Kenya wazamisha Namibia kufuzu Olimpiki magongo

Warembo wa Kenya wazamisha Namibia kufuzu Olimpiki magongo

Na GEOFFREY ANENE

KENYA imeanza kampeni za kutafuta tiketi ya kushiriki mpira wa magongo ya wanawake kwa mara ya kwanza kabisa kwenye Olimpiki kwa kulipua Nambia 1-0 katika mchujo wa Afrika ulioanza nchini Afrika Kusini mnamo Agosti 12, 2019.

Kiungo wa timu ya Chuo Kikuu cha USIU, Grace Makokha alifungia Kenya bao la pekee katika kipindi cha pili baada ya kile cha kwanza kutamatika 0-0. Bao hili lilipatikana baada ya Kenya kupokonya Namibia mpira ikishambulia na kujibu shambulizi hilo kwa haraka katika robo ya tatu.

Kenya ilistahimili mashambulizi makali kutoka kwa Namibia kutoka kipenga cha kwanza hadi mwisho. Namibia ilitawala mchuano huu na kupata kona nne fupi dhidi ya moja kutoka kwa Kenya, ambayo ilitumia nafasi zake chache kuadhibu wapinzani hao wao.

Warembo wa Kenya almaarufu Tausi, ambao wananolewa na kocha Tom Olal, watavaana na Ghana katika mechi yao ijayo Agosti 13, wachapane na Zimbabwe mnamo Agosti 15 na kukamilisha mashindano haya yanayotumia mfumo wa mzunguko dhidi ya miamba Afrika Kusini mnamo Agosti 17.

Timu ya wanaume ya Kenya, ambayo ilishiriki Olimpiki mara ya mwisho mwaka 1988 jijini Seoul nchini Korea Kusini, itaanza kampeni ya kutafuta kurejea katika ulingo huo dhidi ya Ghana baadaye Agosti 12 kabla ya kulimana na Misri (Agosti 13), Zimbabwe (Agosti 15), Afrika Kusini (Agosti 17) na kuikamilisha dhidi ya Namibia (Agosti 18). Washindi wa vitengo hivi viwili pekee ndio watakaoingia Olimpiki jijini Tokyo nchini Japan mwaka ujao.

You can share this post!

Oduor, 20 kusakata soka Uingereza kwa miaka 4

Lionesses na Simbas wasalia katika nafasi zao viwango vya...

adminleo