Wasekao! Gor watwaa taji la 18, kulihifadhi milele
GOR Mahia walidhihirisha uhodari wao Jumatano kwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Kenya (KPL) mapema zikisalia mechi mbili.
Mara tu mechi yao ilipomalizika ugani Kenyatta, Machakos, waliongozwa na nahodha Harun Shakava na mshambuliaji matata Jacques Tuyisenge kuusherehekea ubingwa huo wa 18.
Mashabiki wa K’Ogalo walimwagika uwanjani kujumuika na wachezaji kuufurahia ushindi baada ya mabingwa hao kufikisha pointi 70 na iwapo watashinda mechi zilizobakia dhidi ya Posta Rangers na Mathare, watafikisha pointi 76.
Bandari ambao wamefikisha pointi 62 baada ya kutoka sare 0-0 na Mathare United pia jana ugani Kasarani, wanaweza tu kufikisha pointi 68 hata kama watashinda mechi zao zote mbili zilizosalia dhidi ya Nzoia Sugar na Sofapaka.
“Ninawapongeza wachezaji wote kwa kujitahidi na kuniunga mkono kutimiza ndoto yangu. Nina kikosi ambacho kina uwezo wa kushinda hata ubingwa wa bara iwapo kuna mipango kabambe,” alieleza kocha Hassan Oktay.
Katika mechi ya Jumatano, mabingwa hao walijipatia bao kupitia kwa Charles Momanyi kabla ya Vihiga kusawazisha kupitia kwa Amos Kigadi.
“Nina mpango wa kushinda taji hili, lakini siwezi kifichua siri yangu kwa sababu tunataka tuendelee kulinyakua,” alisema mwenyekiti wao, Ambrose Rachier.
“Huu ulikuwa msimu mgumu zaidi kwetu kwa sababu tulishiriki katika mashindano mengi yaliyofanya baadhi ya wachezaji kuchoka. Tunawapongeza wafadhili wetu SportPesa, mashabiki na washikadau wote wanaofuatilia klabu hii,” aliongeza.
Oktay aliyechukua usukani kutoka kwa Dylan Kerr anayeandaa Black Leopards ya Afrika Kusini, alitoa pongezi zake.
Umekuwa msimu ambao Gor Mahia wamecheza vizuri zaidi kuliko wapinzani wao wa karibu AFC Leopards, Tusker na Ulinzi Stars, ambao wanashikilia nafasi za 10, saba na tisa jedwalini mtawalia.
Kikosi hiki kimeongezwa nguvu na wachezaji wapya wakiwemo Nicholas Kipkurui, Momanyi, Kenneth Muguna na beki wa kushoto, Shafique Batambuze kutoka Uganda. Wengi wanadhania kuwa huenda kuimarika kwao kunatokana na kushiriki kwao mara kwa mara katika mechi za bara ambapo walikutana na timu za hadhi kubwa na hata kushinda baadhi yazo.
Huu ni ushindi wa tatu mfululizo kwa Gor, kumaanisha watahifadhi taji hilo daima na milele, kulingana na kanuni za soka.
AFC Leopards ilikuwa timu ya kwanza kuhifadhi taji hilo daima ilipolishinda mwaka wa 1980, 1981 na 1982.