Waterworks yatwaa ubingwa Nairobi NWRL
Na JOHN KIMWERE
KIKOSI cha wanasoka wa Waterworks FC ndio mabingwa wa ngarambe ya Nairobi West Regional League (NWRL) baada ya kucharaza South B Sportiff FC bao 1-0 katika fainali iliyochezewa uwanja wa Kenya School of Government (KSG) Kabete, Nairobi.
Katika mpango mzima timu zote mbili zimepandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu ujao. Wachezaji wa pande zote waliingia mzigoni wakilenga kuonyesha ubabe wao na kutawazwa wafalme wa ngarambe hiyo.
Timu hizo zilionyesha mchezo safi huku zikitoa mashambalizi ya kweli kutafuta mabao ya mapema kabla ya kuagana sare tasa katika kipindi cha kwanza.
Kipindi cha lala salama wanasoka hao walirejea dimbani kwa kishindo ambapo Waterworks FC itajilaumu vikali baada ya kudondosha nafasi kadhaa ilizopata.
Katika kile kilionyesha kuwa wachezaji hao walitii mawaidha ya kocha, Josiah Okello walifanya kweli na kubeba taji hilo kufuatia bao lililofumwa kimiani na Vitalis Okomo dakika ya 80.
”Nashukuru wenzangu kwa kuonyesha ushirikiano mwema ingawa kiasi wapinzani wetu walionekana kutulemea,” nahodha wa Waterworks, Zuberi Mohamed alisema na kuongeza kuwa baada ya mchezo huo sasa wanageukia maandalizi ya kushiriki Ligi ya Taifa Daraja ya Pili msimu ujao.
Waterworks FC ilishiriki fainali hiyo baada ya kumaliza kidedea kwenye jedwali ya mechi za Kundi A kwa kufikisha alama 27, tatu mbele ya Nairobi Prisons.
Nayo South B Sportiff FC ilikusanya alama 27, moja mbele ya South B Allstars na kumaliza kileleni mwa mechi za Kundi B.