'Wikendi ya manyanyaso miamba ikifukuzana EPL'
Na MASHIRIKA
LONDON, Uingereza
VIONGOZI Liverpool, mabingwa watetezi Manchester City na Chelsea wanatarajiwa kuendeleza nyanyaso zao dhidi ya waonyonge Sheffield United, Everton na Brighton kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) itakayoingia raundi ya saba, leo Jumamosi.
Sheffield watahitaji muujiza katika uwanja wao wa nyumbani wa Bramall Lane dhidi ya Liverpool inayojivunia kupepeta washiriki hao wapya katika mechi 12 zilizopita. Vijana wa kocha Chris Wilder hawana ushindi dhidi ya Liverpool katika mechi tatu zilizopita.
Walipepetwa na Liverpool 4-0 walipokutana mara ya mwisho mwaka wa 2007.
Sheffield United, ambayo ilivunja rekodi ya Everton kushinda mechi sita mfululizo uwanjani Goodison Park ilipoipiga 2-0 Septemba 21, pia inakutana na klabu inayotafuta ushindi wa 16 mfululizo ligini.
Vijana wa Wilder walipoteza mechi zao mbili zilizopita za ligi uwanjani Bramall Lane dhidi ya Leicester na Southampton.
Takwimu hizi ni ushahidi kuwa Sheffield itakuwa na kibarua kigumu kushinda wafalme hao wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA). Hata sare dhidi ya Liverpool itakuwa kama ushindi kwa Sheffield inayoshikilia nafasi ya 10 kwa alama 10 nyuma ya wapinzani hao wao.
Viwango vilivyowekwa na Liverpool na Manchester City msimu uliopita vinamaanisha kuwa kupoteza alama yoyote ni pigo, kwa hivyo Liverpool inayofurahia mwanya wa alama tano dhidi ya vijana wa Pep Guardiola kileleni, itakuwa makini kujiondelea presha kwa kuvuna ushindi.
Sheffield itatumai kupata motisha kutokana na kuwa tangu mwaka 1990, haijapoteza mechi tatu mfululizo za ligi katika uwanja wake wa nyumbani. Pia, Liverpool haijapata ushindi ligini uwanjani Bramall Lane tangu mwaka 1990.
Klopp alifanya mabadiliko 11 katika kikosi kilicholipua Milton Keynes 5-0 katika mashindano ya League Cup katikati ya juma kwa hivyo Liverpool inatarajiwa kukaribisha silaha zake kali kama Virgil van Dijk, Mohamed Salah, Roberto Firmino na Sadio Mane.
Sheffield pia ilifanya mabadiliko mengi ikipoteza 1-0 dhidi ya Sunderland katika League Cup kwa hivyo itatumia wachezaji wake wazuri wakiwemo Callum Robinson, John Lundstram na Oliver McBurnie. Vijana wa Guardiola watazuru uwanjani Goodison Park wakitumai kushinda ili waendelee kuwekea Liverpool presha. Tangu walipoduwazwa 3-2 na Norwich, Manchester City wamemiminia wapinzani vichapo.
Wamefunga mabao 14 katika mechi tatu ikiwemo kubwaga Watford 8-0. Hata hivyo, Everton, ambayo kocha wake Marco Silva anakodolea macho kupigwa kalamu kwa msururu wa matokeo duni, inatarajiwa kuwa mtihani mkali.
Kupoteza
Vijana wa Silva walipoteza mechi tatu zilizopita dhidi ya City kwa hivyo watalenga kulipiza kisasi.
Watatumai kupata makali yaliyowafanya kulemea Manchester United 4-0, Arsenal 1-0 na Chelsea 2-0 uwanjani Goodison Park msimu uliopita. Baadhi ya wachezaji wakali wanaotarajiwa kuvuma ni Mbrazil Richarlison (Everton) na raia wa Argentina, Sergio Aguero (Manchester City).
Nayo Tottenham inayojivunia mvamizi matata Harry Kane, itakuwa mwenyeji wa Southampton. Itatafuta ushindi wake wa nne mfululizo dhidi ya wapinzani hawa uwanjani Tottenham.
Chelsea pia itakuwa nyumbani kuzichapa dhidi ya Brighton. Vijana wa Frank Lampard watakuwa wakifukuzia ushindi wa nne mfululizo dhidi ya Brighton. Arsenal na Manchester United ni Jumatatu.