Willian athibitisha kuagana rasmi na Chelsea
Na CHRIS ADUNGO
KIUNGO mvamizi mzawa wa Brazil, Willian Borges da Silva, 32, amethibitisha kuondoka kambini mwa Chelsea baada ya kuwahudumia kwa kipindi cha miaka saba.
Nyota huyo alikosa kuchezea Chelsea dhidi ya Arsenal katika fainali ya Kombe la FA mnamo Agosti 1, 2020, uwanjani Wembley, Uingereza na akawa nje ya kikosi kilichobanduliwa na Bayern Munich kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Agosti 8, 2020, kwa sababu ya jeraha la kifundo cha mguu.
Kuagana kwake na Chelsea kunachangiwa na kukosekana kwa mwafaka kati yake na usimamizi uliokataa kurefusha mkataba wake kwa miaka mitatu zaidi ugani Stamford Bridge.
Willian kwa sasa anasubiri kuingia katika sajili rasmi ya Arsenal wanaonolewa na kocha Mikel Arteta.
“Muda wa kuondoka sasa ugani Stamford Bridge umewadia. Naondoka Chelsea nikijivunia mambo mengi. Nimenyanyua mataji kadhaa hapa na nimetekeleza yote yaliyonihusu kwa bidii na moyo wa kujitolea,” akasema Willian.
Akiwa mchezaji wa Chelsea, Willian aliwajibishwa mara 339 tangu 2013 alipokatiza uhusiano wake na kikosi cha Anzhi Makhachkala nchini Urusi kwa kima cha Sh4.2 bilioni.
Willian ameongoza Chelsea kunyanyua mataji matano, mawili yakiwa ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na Europa League.
Aliwahi kutawazwa mchezaji bora wa mwaka kambini mwa Chelsea mara mbili.
“Kulikuwa na nyakati nyingi za furaha na chache za masikitiko. Kulikuwa na nyakati za kutwaa mataji na nyingine za kufanya kazi kwa presha uwanjani. Mseto huu wote wa matukio ulileta ukamilifu murua ndani ya kikosi cha Chelsea. Asanteni sana mashabiki wetu na pongezi za pekee kwa vinara walionilea na kunifanya kama mmoja wa watoto wao katika familia pana ya The Blues,” akaongeza Willian.