Wito FKF ishauriane na timu za KPL
Na CHRIS ADUNGO
MWENYEKITI wa Mathare United, Bob Munro amesema klabu za Ligi Kuu ya Kenya ndizo zitakazokuwa na usemi wa mwisho kuhusu mwendeshaji mpya wa kipute hicho iwapo Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) litakatiza uhusiano wake na kampuni ya KPL.
Kwa mujibu wake, klabu 18 za ligi ya humu nchini ndio wadau wakuu katika KPL kwa sasa na itakuwa vyema iwapo FKF itashauriana na wasimamizi wa vikosi hivyo kabla ya kutafuta mwendeshaji mpya wa ligi iwapo itatekeleza tishio la kutorefusha mkataba wa KPL baada ya kutamatika rasmi mnamo Septemba 24, 2020.
Kauli ya Munro ambaye ni miongoni mwa waasisi wa KPL, inatolewa siku mbili baada ya Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Lordvick Aduda kutaka vikosi vyote vya Ligi Kuu ya soka ya humu nchini kupinga vikali jaribio lolote la kuvisajilisha kisiri kwa mwendeshaji ligi tofauti.
Aduda ambaye ni miongoni mwa wawaniaji wa urais wa FKF katika uchaguzi ujao wa kitaifa, amedokeza kuwa upo muungano mpya unaonukia miongoni mwa wawaniaji wa kiti hicho. Muungano huo utamjumuisha yeye, Naibu Rais wa zamani wa FKF Sammy Shollei, Katibu Mkuu wa zamani wa Cecafa Nicholas Musonye, mwaniaji wa zamani wa urais wa FKF Hussein Mohammed, Andrew Amukowa wa eneo la Magharibi ya Kenya na Twaha Mubarak wa Mombasa.
Munro anashikilia kwamba masaibu ya SoNy Sugar waliotupwa nje ya kipute cha KPL mwanzoni mwa msimu huu yalichangiwa na uongozi mbaya wa FKF na mrundiko wa mechi za ugenini uliofyonza hazina yao ya fedha kwa haraka.
Anasikitika kwamba usimamizi mbaya wa FKF ndicho kiini cha kubanduka kwa SuperSport waliokuwa wadhamini wa Ligi Kuu ya humu nchini kwa kipindi kirefu.
Kampuni hiyo ya Afrika Kusini ilikatiza uhusiano na KPL mnamo Aprili 2017 kutokana na msukosuko wa kandarasi baada ya FKF kuongeza washiriki wa Ligi Kuu ya soka ya Kenya hadi klabu 18 badala ya 16.