Yafichuka Barcelona ilikataa huduma za Kylian Mbappe
Na GEOFFREY ANENE
TETESI zinasema kwamba klabu ya Barcelona ilimpuuza kinda matata Kylian Mbappe, ambaye alitamani sana kujiunga nayo na kuichezea msimu huu wa 2018-2019.
Kulingana na vyombo vya habari nchini Uhispania, wakala wa zamani Josep Maria Minguella, ambaye ana uhusiano wa karibu na Barcelona, miamba hawa wa Uhispania hawakujibu ombi la Mbappe ambaye alitamani sana kushirikiana na bingwa mara tano wa tuzo ya mwanasoka duniani (Ballon d’Or), Lionel Messi.
“Mnamo Agosti 5 (mwaka 2018), niliwasilishia Barca mchezaji Mbappe,” alieleza vyombo hivyo vya habari kabla ya kuongeza, “Ombi hilo lilipuuzwa na sasa nadhani ni kosa ambalo Barca itajutia kwa miaka 10 ijayo.”
Mbappe alijiunga na Paris Saint-Germain kutoka AS Monaco baada ya Barca. Ameng’aa kwenye Ligi Kuu ya Ufaransa akiifungia PSG mabao 13 na kumega pasi sita zilizozalisha mabao katika mechi 13 katika mashindano yote.
Alikuwa na kipindi kizuri katika Kombe la Dunia nchini Urusi mwezi Juni na Julai mwaka huu aliposhinda taji na nchi yake ya Ufaransa. Aliifungia mabao manne, mawili nyuma ya mfungaji bora Harry Kane wa Uingereza.