Michezo

Zidane asema anastahili lawama kwa kichapo cha 3-2 ambacho Real Madrid walipokezwa na Shakhtar Donetsk katika UEFA

October 23rd, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

KOCHA Zinedine Zidane amesema kwamba ndiye anayestahili kulaumiwa kwa kichapo cha 3-2 ambacho kikosi chake cha Real Madrid kilipokezwa na Shakhtar Donetsk ya Ukraine kwenye mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Oktoba 21, 2020,F ugani Alfredo di Stefano.

Donetsk ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Ukraine walitua jijini Madrid wakikosa huduma za wanasoka 13 wa kikosi cha kwanza baada ya visa vya maambukizi ya virusi vya corona kuripotiwa kambini mwao.

Hali hiyo ilimweka kocha Luis Castro wa Donetsk katika ulazima wa kutegemea kikosi chake cha wachezaji chipukizi dhidi ya Madrid ambao ni wafalme mara 13 wa taji la UEFA.

Tineja Cardoso Lemos Martins aliwafungulia Donetsk ukurasa wa mabao kunako dakika ya 29 kabla ya beki Raphael Varane kujifunga dakika nne baadaye. Fowadi Manor Solomon alifanya mambo kuwa 3-0 kwa upande wa Donetsk kufikia mwisho wa kipindi cha kwanza.

Ingawa Luka Modric na Vinicius Junior walirejesha Real mchezoni katika kipindi cha pili, jitihada zao miamba hao wa soka ya Uhispania hazikuyumbisha uthabiti wa Donetsk ambao licha ya kuchezea ugenini na kutegemea kikosi cha vijana wa umri mdogo, walisalia walizidi kushambulia na kutatiza mabeki wa Real hadi dakika za mwisho.

Japo Federico Valverde alidhani kuwa alikuwa amesawazishia Real mwishoni mwa kipindi cha pili, refa Srdjan Jovanovic hakuhesabu bao lake baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alikuwa ameotea.

Kichapo ambacho Real walipokezwa kilitokea siku tatu baada ya kuduwazwa tena na limbukeni Cadiz waliowapepeta 1-0 kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Akidhibiti mikoba ya Real katika awamu ya kwanza ya kuhudumu kwake ugani Santiago Bernabeu, kocha Zidane aliwaongoza miamba hao kutwaa ubingwa wa UEFA kwa misimu mitatu mfululizo.

Akihojiwa na wanahabari mwishoni mwa mechi yao na Donetsk, Zidane alikiri kwamba mojawapo ya sababu zilizomsukuma kupumzisha baadhi ya wanasoka wake tegemeo katika mchuano huo ni haja ya kujiweka pazuri zaidi kwa gozi la El Clasico dhidi ya Barcelona uwanjani Camp Nou mnamo Oktoba 24.

Bila ya huduma za beki na nahodha Sergio Ramos aliyepata jeraha dhidi ya Cadiz, Real walitepetea sana kwenye safu ya ulinzi baada ya mabeki wao kushindwa kuzima makali ya Mateus Tete na Manor Solomon.

Real kwa sasa wamepoteza mechi saba kati ya nane zilizopita bila ya Ramos kuwa katika safu yao ya nyuma.

Ilikuwa mara ya kwanza tangu Septemba 1986 kwa Real kupoteza mechi tatu mfululizo za UEFA.

Kwa upande wao, Donetsk ni kikosi cha kwanza kutoka Ukraine kuwahi kubwaga Real kwenye gozi la UEFA tangu Machi 1999 walipopokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Dynamo Kiev. Kiev waliposajili ushindi huo dhidi ya Real, wafungaji wawili wa Donetsk, Manor (Julai 1999) na Tete (Februari 2000) hawakuwa wamezaliwa.

Varane aliweka rekodi ya kuwa mchezaji wa tatu wa Real baad aya Ivan Helguera na Sergio Ramos kuwahi kujifunga kwenye gozi la UEFA.

Bao ambalo Vinicius alifungia Real sekunde 15 pekee baada ya kutokea benchi ndilo la haraka zaidi kuwahi kushuhudiwa kwenye kivumbi cha UEFA tangu 2006-07. Luka Modric sasa ndiye mwanasoka wa nne baada ya Alfredo Di Stefano, Ferenc Puskas na Paco Gento kuwahi kufungia Real wakijivunia umri wa zaidi ya miaka 35 na zaidi.

Kwingineko, mechi hiyo ilimpa Anatolii Trubin, 19, fursa ya kuwa kipa wa pili mwenye umri mdogo zaidi baada ya Timon Wellenreuther wa Schalke kuwahi kuanzishwa kwenye mechi dhidi ya Real. Wellenreuther aliwahi kuchezeshwa na Schalke ya Ujerumani dhidi ya Real mnamo 2015 akiwa na umri wa miaka 19 na siku 77 pekee.