• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
Zidane asema hatajiuzulu licha ya Real Madrid kupigwa tena na Shakhtar Donetsk kwenye UEFA

Zidane asema hatajiuzulu licha ya Real Madrid kupigwa tena na Shakhtar Donetsk kwenye UEFA

Na MASHIRIKA

KOCHA Zinedine Zidane wa Real Madrid amesema kwamba “hatajiuzulu” licha ya kikosi chake kupokezwa kichapo cha 2-0 kutoka kwa Shakhtar Donetsk ya Ukraine na kudidimiza matumaini ya kusonga mbele kwa mabingwa hao watetezi wa soka ya Uhispania kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu.

Real ambao ni wafalme mara 13 wa UEFA, sasa wana ulazima wa kupiga Borussia Monchengladbach katika mchuano wao wa mwisho wa Kundi B ili kufuzu kwa hatua ya mwondoano.

“Siendi kujiuzulu. Sitajiuzulu kabisa. Tunapitia hali ngumu na hili ni jambo la kawaida. Lakini nina imani tele kwamba tutajinyanyua na matokeo duni tunayoshuhudia kwa sasa kikosini litakuwa suala la kuzikika na kusahaulika,” akatanguliza Zidane.

Kocha huyo raia wa Ufaransa aliongoza kikosi chake kucheza na Donetsk siku tatu baada ya Real kupigwa 2-1 na Alaves kwenye Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) katika uwanja wa nyumbani wa Alfredo di Stefano.

“Nina nguvu, ujuzi, uwezo na maarifa ya kugeuza mambo kambini na kurejesha kikosi cha Real kinapostahili kuwa. Nitafanya kila kitu kilichoko ndani ya uwezo wangu kunyoosha mambo. Naamini wachezaji nao wamechoka na kukosolewa mara kwa mara na kulaumiwa. Sina shaka wataniunga mkono kwa hili,” akasema Zidane ambaye ni mchezaji wa zamani wa Real.

Ilikuwa mara ya pili kwa Real kupoteza mechi dhidi ya Donetsk waliowachapa 3-2 katika mchuano wa mkondo wa kwanza jijini Madrid mnamo Oktoba 2020.

Masaibu ya Real katika Kundi B yalizidishwa na ushindi wa 3-2 uliosajiliwa na Inter Milan dhidi ya Borussia Monchengladbach ya Ujerumani katika mchuano mwingine wa Disemba 1, 2020. Inter ya kocha Antonio Conte ilifungiwa mabao mawili na fowadi wa zamani wa Everton na Manchester United, Romelu Lukaku.

Real ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne kwenye msimamo wa jedwali la La Liga, walishuka dimbani kuvaana na Donetsk bila ya huduma za fowadi Eden Hazard na nahodha Sergio Ramos.

Hata hivyo, walitumia mchuano huo kumkaribisha kikosini mshambuliaji Karim Benzema aliyechangia bao lao la ushindi dhidi ya Liverpool mnamo 2018 na kutwaa ubingwa wa UEFA nchini Ukraine.

Licha ya Real kuanza vizuri kwa kushambulia sana kupitia kwa Marco Asensio na Benzema, juhudi zao hazikuzaa matunda huku kipa Anatoliy Trubin akijituma maradufu langoni mwa Donetsk. Real kwa sasa wamesajili ushindi mara nne pekee kutokana na mechi 11 zilizopita katika mashindano yote.

Mechi mbili ambazo Real wamepoteza hadi kufikia sasa kwenye makundi ya UEFA ndiyo idadi kubwa zaidi kwa kikosi hicho kuwahi kupoteza tangu 2016-17, 2017-18 na 2019-20 ambapo walipigwa mara mbili pekee kutokana na jumla ya mechi 18.

Donetsk wameshinda mechi mbili pekee kati ya tisa zilizopita kwenye UEFA msimu huu, nazo zimekuwa dhidi ya Real Madrid.

You can share this post!

Ripoti ya ‘Production Gap’ yapendekeza mataifa...

Liverpool wapiga Ajax na kusonga mbele UEFA huku chipukizi...