Habari

Mji wa Ruiru kunufaika na ukarabati wa barabara wa Sh4 bilioni

June 15th, 2019 1 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Ruiru watanufaika pakubwa na ukarabati wa barabara za mji huo kuunganishwa na ile ya kwenda Githunguri hadi Uplands.

Waziri wa Barabara na Miundomsingi Bw James Macharia alizuru mji wa Ruiru mnamo Ijumaa ili kuzindua barabara itakayogharimu takribani Sh4 bilioni.

Alisema vivukio vya daraja pia vitawekwa katika maeneo tofauti ambapo kwa miezi michache ijayo, kazi hiyo itakuwa imekamilika.

Alisema mji wa Ruiru umepiga hatua kubwa kimaendeleo na kwa hivyo ni vyema pia kupata miundomsingi ya kisasa ambapo sasa barabara ya Uplands itaunga hadi kwenye barabara kuu ya Nairobi-Nakuru.

Hata hivyo, alisema barabara inayoelekea Githunguri imechukua muda mrefu kukamilika huku akiwahimiza wahandisi katika mradi huo wafanye hima waikamilishe haraka iwezekanavyo ili wananchi wazidi kupanua biashara zao.

“Ningetaka kuona ya kwamba barabara hii ya kutoka Ruiru kuelekea Githunguri hadi Uplands ikikamilika haraka iwezekanavyo kwa sababu imechukua sasa muda mrefu ajabu,” alisema Bw Macharia aliyeandamana na mbunge wa Ruiru, Bw Simon King’ara.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara (kulia ) azungumza na waziri James Macharia. Picha/ Lawrence Ongaro

Alisema angetaka kuona ya kwamba ifikapo mwaka wa 2021 vivukio hivyo vimejengwa katika maeneo yote muhimu ili wananchi wapate nafasi ya kupita kwa urahisi bila kupata ajali za kila mara.

Alisema barabara hiyo ni muhimu sana kwa sababu itaweza kuunganisha kaunti nne na pia itaunganisha mataifa jirani ya Somalia, Uganda, na Tanzania.

“Hii ni njia moja ya kuboresha biashara miongoni mwa nchi hizo jirani huku wananchi wakijumuika pamoja kuendeleza biashara zao,” alisema Bw Macharia.

Mbunge wa Ruiru Bw King’ara alisema mji wa Ruiru utapiga hatua kubwa kwa miundomsingi kwa sababu barabara ya kutoka kiwanda cha misumari cha Devick hadi maeneo ya Railways itakamilika hivi karibuni baadaye itaelekezwa hadi Uplands ambapo itaweza kushikanisha Superhighway ya kuelekea Nakuru kutoka jijini Nairobi.

“Ninashukuru hatua nzuri ambayo serikali imechukua ya kukarabati barabara za mji wa Ruiru na za kuunganisha maeneo mengine,” alisema Bw Kinga’ra.