Habari za Kitaifa

Mkasa wa Endarasha: Wanafunzi 21 wafariki 48 wakitafutwa na serikali


IDADI ya wanafunzi waliokufa katika mkasa wa moto shuleni Hillside Endarasha Academy, Nyeri imepanda hadi 21 na kuna hofu zaidi wengine wakitoweka.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Jumamosi jioni Msemaji wa Serikali Isaac Mwaura alisema mili 19 ilipatikana eneo la mkasa huku wanafunzi wawili wakifa wakati wanapokea matibabu hospitalini.

“Kupitia usaidizi wa maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) na mwanapatholojia wa serikali, mili 19 ilipatikana katika bweni lililoteketea. Wanafunzi wawili zaidi walikufa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta na Hospitali ya Mary Immaculate, Nyeri,” akasema.

“Mkasa huu ambapo watoto wetu 21 walikufa kufuatia mkasa wa moto katika bweni la wavulana katika Shule ya Hillside Endarasha Academy ni mbaya zaidi. Bweni hilo lilikuwa na wanafunzi 156,” Bw Mwaura akaongeza.

Taarifa hiyo ilitolewa baada ya maafisa wakuu wa serikali wakiongozwa na Waziri wa Elimu Julius Ogamba kuzuru shule hiyo iliyoko eneo bunge la Kieni.

Waziri huyo aliandamana na Katibu wa Wizara anayesimamia Elimu ya Msingi Belio Kipsang’.

Mkasa huo ulitokea Alhamisi mwendo wa saa tano za usiku.

Utambuzi wa wapendwa

Taasisi za huduma za dharura kama vile Shirika la Msalaba mwekundu na taasisi nyingine za serikali kuu pamoja na ile ya kaunti ya Nyeri, zimebuni kitengo maalumu cha misaada.

Wanalenga kuwasaidia wazazi, ndugu na jamaa wa wanafunzi hao kuwatambua watoto wao, na kutoa taarifa muhimu kuhusu mkasa huo.

Akizungumza na kituo cha habari cha Aljazeera, msemaji wa serikali alisema wanafunzi 48 ‘hawajulikani walipo’.

“Tumewapata wavulana 108 kati ya 156. Tungali tunatafuta wavulana 48,” alisema Jumamosi jioni.

Serikali inaomba wazazi wawapeleke watoto wao shuleni ili wahesabiwe kufuatia mkanganyiko uliosababaishwa na mkasa huo wa moto.