Makala

MOI DEI: Baada ya miaka 24, Moi aliomba Wakenya msamaha

October 11th, 2018 2 min read

Na PETER MBURU

KUREJEA kwa sikukuu ya Moi Dei baada ya kufutiliwa wakati katiba mpya ya 2010 ilipoidhinishwa kunaleta tena kumbukumbu za Rais wa pili wa jamhuri ya Kenya, Mzee Daniel Arap Moi, utawala wake wa miaka 24 na namna alivyoondoka uongozini.

Huenda vijana wengi wasiwe na ufahamu mzuri wa Rais Moi na namna alivyoongoza Kenya kati ya 1978 na 2002, kwani wengi wamekuwa wakisikia tu kumhusu ama kufuatilia habari za uzee uliomzonga sasa.

Sikukuu ya Moi Day ilianzishwa mnamo 1989 ili kusherehekea Rais huyo wa pili wa taifa, aliyeongoza baada ya Rais mwanzilishi Mzee Jomo Kenyatta kuaga dunia Agosti 20, 1978.

Mzee Moi aliingia uongozini katika hali iliyowashangaza wengi kwani hakutarajiwa, wakati wa uongozi wake akikumbwa na vizingiti tele kutoka kwa baadhi ya viongozi ambao hawakumtaka kuongoza, pamoja na kukosolewa na watu na makundi yaliyodai utawala wake ulikuwa wa kiimla.

Hata hivyo, kuna wengine waliompenda haswa kufuatia sera zake za kuinua sekta ya elimu kama kuwapa watoto wa shule maziwa, ‘Maziwa ya Nyayo’ kwa kipindi cha miaka 20, sera ambayo iliinua idadi ya watoto waliosoma kutoka 2.9 hadi 3.6milioni kati ya 1978 na 1979.

Hadi wakati wa kustaafu kwake, pingamizi dhidi ya utawala wa Mzee Moi ilikuwa imezidi kiwango cha kumfanya atupiwe vifaa na matope katika sherehe ya kumwapisha Rais aliyechukua hatamu baada yake 2002, Rais Mustaafu Mwai Kibaki.

Vilevile, katika sherehe hiyo ya Desemba 30, 2002 Mzee Moi aliwasili katika bustani ya Uhuru Park kwa sherehe ya kumpokeza Mzee Kibaki mamlaka akiwa peke yake, kwa kuwa alifahamu pingamizi walizokuwa nazo wananchi dhidi yake.

Alichukiwa na wengi waliomwona kutawala kidikteta na kujaribu kuwalazimishia kiongozi mridhi, alipompendekeza Rais Uhuru Kenyatta. Baadaye, Bw Kenyatta alipoteza kiti hicho kwa Bw Kibaki.

Lakini licha ya hayo yote, wakati huo wa kumpokeza mamlaka Rais Kibaki, katika hotuba yake ya mwisho kama Rais alizungumza kwa busara, na maneno yake yameishi kukumbukwa kutokana na ushauri aliotoa kwa Wakenya na ambao umeishi kurudiwa, ukivutia wananchi wengi.

Mzee Moi mnamo 2002 alisema “Nilisema mwaka wa tisaini na nane kuwa nitastaafu kipindi hiki cha miaka mitano kikiisha, wengine hawakuamini kwa sababu wanaamini kuwa katika bara la Afrika hakuna mtu anaweza kuwacha uongozi wa Urais.

“Uongozi uko kwa wananchi, na sisi tu ni wadhamini wao, na ndio maana nataka kuwaambia wananchi ambao wanatafuta demokrasia, tafadhali tafadhali muwe na msimamo wa kuamini yale mnayoyaamini, haiwezekani kiongozi kuraka haopa, kesho hapa.”

“Uwe unaamini kwamba naingia chama cha KANU kwa sababu gani, huingii tui kwa sababu ni chama cha KANU, lazima uangalie kwa makini muongozo wa KANU ni nini na unasema chama hiki kinanifaa na nitakaa hapo hapo, hata kukiwapo nini.”

“Nasema hivi kwa sababu nitaondoka kwa siasa za majibizano, niwe raia mwema, lakini wale wanaozingatia kuongoza, msiweke Kenya chini, msiweke msingi wa siasa zenu kwa chuki,” Mzee Moi akaendelea.

Alizidi kuwaomba radhi wote kabla ya kuondoka kwenye kiti akisema “Kama kuna mtu amenikosea namsamehe, na kama yuko mtu ambaye nimesema chochote ambacho kimechoma roho yake, unisamehe.”

Sherehe ya Moi Dei ya mwisho katika utawala wake, Rais Moi aliisherehekea katika makao ya watoto wasio na makwao, eneo la Thika.

Inasemekana kuwa Mzee Moi, ambaye alizaliwa mnamo 1924 alipelekwa shuleni kutokana na uvivu wa kuchunga mifugo wa wazazi na hali kuwa kila alipoenda malishoni alikuwa akiwapoteza baadhi ya mifugo.

Hali hii iliwafanya wazazi wake kumpendekeza akasome wakati wamishenali walipoingia na kuanza kutafuta watoto wa kuwasomesha.