Habari za Kitaifa

Mshukiwa mkuu wa mlipuko wa gesi Embakasi akamatwa

February 6th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

MSHUKIWA mkuu wa kituo cha kujaza gesi katika mitungi katika eneo la Mradi, Embakasi kulikotokea mlipuko mkubwa mnamo Alhamisi usiku na kusababisha vifo vya watu sita huku 300 wakijeruhiwa, amekamatwa.

Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) imesema Jumanne kwamba Bw Derrick Kimathi amekamatwa huku ikiendelea kuwasaka washukiwa watano zaidi kuhusiana na mkasa huo wa mlipuko wa gesi.

Soma Pia: Mwekezaji katika eneo la mlipuko wa gesi azungumza kupitia mawakili wake

Kwenye taarifa, idara hiyo iliwataja washukiwa hao watano kuwa ni Stephen Kilonzo (msimamizi mkuu wa kituo hicho), Ann Kabiri Mirungi (mfanyakazi wa Namlaka ya Kuhifadhi Mazingira Nchini – Nema), Lynette Cheruiyot (Afisa wa Ngazi za Juu wa Mazingira-Nema), Robert Gitau na Abraham Mwangi (ambao ni madereva).

Idara hiyo ilisema kuwa watano hao bado wako mafichoni na wanatakikana ili kujibu maswali kuhusu “makosa waliyofanya ambayo yamesababisha mahangaiko na mateso mengi kwa Wakenya wenzao”.

Idara ilisema kuwa yeyote ambaye na maelezo yoyote kuhusu waliko washukiwa hao anafaa kuifahamamisha kupitia nambari ya simu 08000722203 au kuripoti katika kituo chochote cha polisi.

Baadhi ya waathiriwa waliopata majeraha wametibiwa na kuruhusiwa kuenda nyumbani, kulingana na taarifa zilizotolewa na Serikali ya Kaunti ya Nairobi.

Mnamo Jumatatu baadhi ya waathiriwa katika vituo vya redio nchini walielezea namna walivyokumbana na mkasa huo, huku wakielezea kuhusu mchakato wa matibabu.

Walimtaja Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nairobi Esther Passaris alitajwa pakubwa kwamba alitoa mchango muhimu kuhakikisha majeruhi wanapata matibabu.

Baadhi ya hospitali ambazo zimekuwa zikiwashughulikia wagonjwa hao ni Mama Lucy Kibaki Hospital, na Hospitali ya Utafiti, Mafunzo na Rufaa ya Chuo Kikuu cha Kenyatta.