Makala

Mshukiwa wa mauaji Kware ameangamiza zaidi ya wanawake 40

Na SAMMY WAWERU July 15th, 2024 1 min read

IDARA ya Upelelezi wa Jinai na Uhalifu (DCI) Jumatatu, Julai 15, 2024 imetangaza kwamba mshukiwa mkuu wa mauaji eneo la Kware, Mukuru Kwa Njenga, Nairobi amekiri kuangamiza zaidi ya wanawake 40.

DCI kwenye kikao na waandishi wa habari katika makao makuu yake, Kiambu Road, imefichua majina ya mshukiwa huyo anayetambulika kama Collins Jumaisha.

Mkurugenzi Mkuu wa DCI, Mohammed Amin amedokeza kwamba kati ya 2020 hadi mwaka huu, 2024, Collins amekiri kuua wanawake 42 akiwemo mkewe, Imelda Judith.

“Mkewe alikuwa mwathiriwa wa kwanza, aligongwa (kwa kifaa butu) hadi akafa,” DCI Amin akasema.

Collins alitiwa nguvuni usiku wa kuamkia Jumatatu (Julai 15, 2024) eneo la Kayole, Nairobi.

Alikamatwa wakati akitazama finali za kipute cha Kandanda cha Bara Uropa.

Kamata kamata hiyo imefanyika baada ya kuopolewa kwa miili 13, kufikia Jumapili, Julai 14 eneo la Kware.

Aidha, miili iliyotolewa kwenye handaki hilo hatari ni ya wanawake, Bw Amin akisema uchunguzi wa mwanzo unaonyesha dalili sawa kwa wote jinsi walivyouawa.

“Uchunguzi wa mwanzo unaonyesha alitumia ujanja unaofanana kuangamiza waathiriwa,” DCI Amin alielezea, akidokeza kwamba tayari makachero wametwaa vifaa alivyotumia kutekeleza uhalifu huo.

Bw Amin alikuwa ameandamana na Kaimu Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, Douglas Kanja.

Collins ametajwa kama mshukiwa haini asiye na utu kwa binadamu.

Hadi kubambwa kwake, inasemekana alikuwa katika harakati za kupanga mahesabu kuangamiza mwanamke mwingine kwa jina Susan.

Aidha, alikamatwa kupitia uchunguzi wa usambazaji wa pesa kwa njia ya simu kwa mwanamke.

Miili iliyoopolewa ilikuwa imefungwa kwenye magunia.

Akipasua kimya chake kuhusu mauaji hayo yanayoashiria huenda yakawa ya halaiki, Rais William Ruto alisema serikali yake itahakikisha washukiwa wameadhibiwa vikali kisheria.

Eneo la Kware sasa limetwaliwa na maafisa wa polisi, uopoaji wa miili zaidi na uchunguzi ukiendelea.