Habari za Kaunti

Mshukiwa mkuu wa mauaji ya meneja wa supamaketi anyakwa

June 6th, 2024 2 min read

NA MERCY KOSKEI

MAAFISA wa usalama katika Kaunti ya Nakuru wanamzuilia mshukiwa mkuu wa mauaji ya meneja wa dukakuu la Chandarama kaunti ndogo ya Naivasha aliyeuawa wiki mbili zilizopita.

Mwili wa Hassan Abdullatif Salim ulipatikana nyumbani kwake ukiwa na majeraha.

Kulingana na kamanda wa polisi kaunti ndogo ya Naivasha Stephen Kirui, mshukiwa Bw Joseph Mungai, alinaswa akiwa mafichoni katika mji wa Naivasha mnamo Jumatano jioni.

Bw Kirui alisema kuwa mshukiwa huyo mwenye umri wa miaka 25 alinaswa na maafisa wa upelelezi kwa msaada wa mwananchi ambaye alijitolea kutoa taarifa hadi kukamatwa kwake.

Bw Mungai alikamatwa katika duka lake la kutengenezea simu za rununu. Katika nyumba ya mshukiwa, wapelelezi walifanikiwa kupata vitu vinavyoaminika kuwa viliibwa kutoka kwa nyumba ya marehemu.

Alipatikana akiwa na televisheni, mtungi wa gesi ya kupikia aina ya Pro Gas wa kilo sita, vitu ambavyo vinashukiwa kuwa mali ya marehemu.

“Wakati wa uchunguzi wetu kuna mtu ambaye alijitolea kutoa taarifa kuwa walikuwa wakionekana pamoja mara kwa mara na kwamba baada ya mauaji hayo kutokea, mshukiwa alibadilisha nguo na kuvaa za marehemu na kwamba nguo zake pia zilikuwa na damu,” alisema.

Mshukiwa huyo anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Naivasha.

Mwili wa Abdullatif ulipatikana ndani ya chumba chake cha kulala ukiwa umelowa damu huku ukiwa na majeraha makubwa matatu kichwani saa chache baada ya kutoka kazini.

Alikuwa ameabiri pikipiki alipofunga supamaketi mwendo wa saa tatu usiku na kufika nyumbani kwake dakika 20 baadaye.

Wafanyakazi wa Chandaria waliingiwa na wasiwasi baada ya Abdullatif kushindwa kuripoti kazini kesho yake kwani yeye ndiye hufunga na kufungua dukakuu hilo.

Baada ya kumsubiri kwa muda wa zaidi ya saa mbili, waliamua kufika nyumbani kwake.

Hata hivyo, mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani. Walijaribu kumpigia simu lakini hakupokea.

Lakini walipata friji na stendi ya televisheni ambayo ilikuwa imeachwa nje, na pia kulikuwa na matone ya damu mlangoni na kuwalazimu kuripoti kwa maafisa wa polisi.