Makala

Msururu wa migomo unavyotikisa Kenya Kwanza


KATIKA miaka miwili ambayo Rais William Ruto amekuwa uongozini, serikali yake imekumbwa na migomo kadhaa wafanyakazi wa sekta mbali mbali wakilalamikia mazingira duni ya kazi na kutotimizwa kwa ahadi na mikataba ya kuongezewa mishahara.

Wakati wa kampeni, Rais Ruto alitoa ahadi kadhaa ikiwa ni pamoja na kuboresha na kushughulikia masilahi ya wafanyakazi katika sekta mbalimbali nchini.

Hata hivyo, ahadi hizi hazijatimizwa kwani chini ya miaka miwili, serikali yake imekumbwa na mgomo baada ya mgomo wafanyakazi wakilalamika.

Jumatano, wahadhiri na wafanyakazi wengine wa vyuo vikuu vya umma nchini walianza mgomo baada ya kutoa ilani ya siku saba.

Mgomo huo umeathiri masomo katika vyuo vikuu vya umma 35.

Chama cha Wahadhiri wa Vyuo Vikuu (Uasu) na Chama cha wafanyakazi wa vyuoni (Kusu) vilisema kuwa hakuna masomo yatakayoendelea katika vyuo vikuu vya umma.

Viongozi wa vyama hivyo walielezea kufadhaika kwao kutokana na kucheleweshwa kwa mazungumzo ya Mkataba wa Makubaliano ya Pamoja wa 2021-2025 na serikali.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi wa mgomo huo katika Chuo Kikuu cha Kiufundi cha Kenya jijini Nairobi, viongozi wa Uasu na Kusu walisema hawatakubali kupokea malipo ya chini, kucheleweshwa kwa malipo, kutowasilishwa kwa makato ya kisheria na kushindwa kwa serikali kutekeleza kikamilifu bima ya matibabu.

“Tuko tayari kwa mazungumzo, lakini hatutarudi kazini hadi makubaliano yaafikiwe. Watie saini makubaliano ya nyongeza ya mishahara ya 2021-2025 au itakuwa mwisho wa dunia,’ alisema Katibu Mkuu wa Uasu Constantine Wasonga.

Mnamo Jumatano, Mahakama Kuu ilisitisha mgomo huo na kutaka pande husika kurudi katika meza ya mazungumzo.

Mfumo wa ufadhili vyuoni

Haya yanajiri tu wiki chache baada ya mgomo kushuhudiwa katika vyuo vikuu mbalimbali wanafunzi wakipinga mfumo mpya wa ufadhili.

Mgomo huo ulioshuhudiwa katika taasisi mbalimbali za elimu ya juu ulimlazimisha Rais Ruto mnamo Septemba 16 kuteua kamati ya watu 129 kushughulikia mfumo wa kufadhili elimu ya vyuo vikuu ambao umeshutumiwa vikali ukidaiwa kuongeza gharama ya elimu na kuwatenga wanafunzi kutoka familia maskini.

Mgomo wa wafanyakazi wa angatua

Mgomo huo ulijiri siku chache baada ya wafanyakazi wa viwanja vya ndege kugoma kulalamikia mpango tata wa serikali ya kukodisha uwanja kimataifa wa ndege wa Jomo Kenyatta kwa kampuni ya India, Adani Enterprises.

Agosti mwaka huu, walimu chini ya Chama cha Kutetea Masilahi ya Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (Kuppet) pia waligoma, jambo ambalo liliathiri masomo katika baadhi ya shule za umma nchini.

Tume ya Huduma za Walimu (TSC) ilizima mgomo huo Septemba 2, 2024, japo baadhi ya wanachama wa Kuppet walionyehsa kutoridhishwa kwao na mkataba wa kurudi kazini.

Wakati huo, Chama cha walimu wa shule za msingi (Knut) kiliitisha mgomo ambao kilifuta dakika ya mwisho.

Watumishi wa umma

Mapema mwezi huu, watumishi wa umma pia walifuta mgomo walioitisha dakika za mwisho.

Hata hivyo, wenzao wa serikali za kaunti wametishia kugoma Septemba 24 iwapo matakwa yao hayatakuwa yametimizwa.

Chama cha Madaktari pia kimeitisha mgomo wa wanachama wake katika baadhi ya kaunti iwapo maslahi yao hayatashughulikiwa.

Kando na hayo, mnamo Machi, serikali ya Kenya kwanza pia ilikumbwa na mgomo wa wauguzi na madaktari uliodumu kwa zaidi ya miezi miwili.

Wauguzi na madaktari hao waligoma wakitaka waongezewe mishahara na kupandishwa vyeo.

Mnamo Juni, utawala wa Rais Ruto ulikumbwa na wimbi jipya la mgomo kutoka kwa vijana wa Gen Z waliojitokeza kwa wingi kupinga Mswada wa Fedha 2024 jambo ambalo lilimfanya rais kuutupilia mbali mswada huo na hata kuwatimua mawaziri wake wote.

Maafisa wa utabibu na wataalamu wa maabara ya matibabu pia waligoma Aprili wakilalamikia masuala sawa na ya madaktari.

Mgomo huo uliathiri huduma za matibabu katika hospitali za umma kote nchini.