Habari Mseto

Mswada unaokinga mawaziri wa kaunti wasifutwe wasukwa

June 7th, 2024 1 min read

Na ERIC MATARA

KUMWONDOA waziri wa kaunti mamlakani itakuwa kibarua kizito kwa madiwani iwapo Seneti itapitishwa Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Serikali ya Kaunti, 2024.

Mswada huo ambao unadhaminiwa na Seneta wa Nandi Samson Cherargei unalenga kukaza kanuni za kumwondoa waziri anayehudumu kwenye kaunti mamlakani pamoja na maafisa wengine wa kaunti.

Mswada huo unalenga kuwakinga maafisa hao kutokana na udhibiti wa madiwani ambao wakati mwingine huwasilisha hoja ya kuwatimua. Hoja za kuwatimua mawaziri au maafisa wa kaunti wakati mwingine huongozwa na shinikizo za kisiasa.

Katika katiba ya sasa, waziri wa kaunti ataondolewa mamlakani iwapo theluthi moja ya madiwani watapiga kura kuunga kutimuliwa kwake.

Mswada wa Bw Cherargei unapendekeza kuwa idadi hiyo iongezwe hadi theluthi mbili kama tu ilivyo kwa mawaziri ambao wanahudumu katika serikali kuu.

Mswada huo tayari umewasilishwa kwa Seneti na Bunge la Kitaifa ili usomwe kwa mara ya kwanza.

“Mswada huo unapendekeza kuimarishwa kwa sheria ya kuwaondoa mawaziri wa kaunti na maafisa wengine. Idadi ya madiwani wa kuwatimua itapanda kutoka theluthi moja hadi theluthi mbili kwa sababu idadi ya sasa ipo chini mno,” ikasema sehemu ya mswada huo.

Mawaziri wengi wa kaunti wamekabiliwa na hoja ya kuwatimua tangu kuanzishwa kwa mfumo wa utawala wa ugatuzi. Hivi majuzu, kulikuwa na hoja ya kumtimua Katibu wa Kaunti ya Nakuru Dkt Samuel Mwaura ambaye huketi katika baraza la mawaziri lakini haikufaulu.

Mnamo Oktoba 25, 2023 madiwani wa Baringo nao walijaribu kumwondoa waziri wa barabara kwa kutonyoa ndevu zake. Hoja hiyo iliwasilishwa na Diwani wa Kisanana Jacob Cheboiwo.